Jan 25, 2024 11:13 UTC
  • Mahakama ya Juu Comoro 'yabariki' ushindi wa Rais Azali Assoumani

Mahakama ya Juu ya Comoro imesema Rais Azali Assoumani alichaguliwa kihalali katika uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita.

Rafik Mohamed, Rais wa Mahakama ya Juu ya Comoro jana Jumatano alitangaza kwa niaba ya majaji wengine wa korti hiyo kuwa Assoumani aliibuka mshindi halali wa uchaguzi wa rais, kama ilivyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya visiwa hivyo vya Bahari Hindi.

Mahakama hiyo ya kilele ya visiwa vya Ngazija imesema Rais Azali Assoumani alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 57.2 ya kura, katika hali ambayo Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo (CENI) ilitangaza kuwa amepata asilimia 62.97 ya kura.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, watu 191,297, sawa na asilimia 57 ya wapiga kura waliosajiliwa, walishiriki kwenye zoezi hilo la kidemokrasia. Uchaguzi wa Comoro ulifanyika Jumapili iliyopita. 

Wagombea watano wa upinzani katika uchaguzi huo walipinga matokeo hayo wakisema zoezi la upigaji kura lilikumbwa na "udanganyifu" na "kujaza masanduku ya kura". Mtu mmoja aliuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika maandamano ya wapinzani ya kupinga matokeo hayo katika mji mkuu Moroni.

Ghasia za baada ya uchaguzi Comoro

Rais Assoumani (65), ambaye amekuwa akituhumiwa kuwakandamiza wapinzani wake kwa mkono wa chuma ikiwemo kuwafunga jela na kuwalazimisha wengine kwenda uhamishoni, alikanusha madai ya kuweko dosari kwenye uchaguzi huo.

Assoumani ambaye anatawala visiwa vya Comoro tangu mwaka 2016 alirefusha muhula wake madarakani kupitia mabadiliko tata ya katiba ya mwaka 2018. Mabadiliko hayo ya katiba yaliyondoa sharti la nafasi ya urais kuwa ya kupokezana miongoni mwa visiwa vitatu vikubwa vinavyounda Jamhuri ya Comoro. 

Assoumani ambaye ni afisa wa zamani wa jeshi, amewahi tena kuingoza Comoro huko nyuma, baina ya mwaka 2002 na 2006.

Tags