Chama cha upinzani chataka kuakhirishwa uchaguzi wa rais Senegal
Chama cha Democratic cha Senegal (PDS) kimewasilisha muswada Bungeni unaotaka kuakirishwa uchaguzi wa rais ulioratibiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Chama hicho cha rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdoulaye Wade hata hivyo hakijapendekeza tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi huo.
PDS imesema katika taarifa kuwa, sababu za kutaka kuakhirishwa kwa uchaguzi huo ni kujiri matukio 'fulani' ambayo yanatishia uwazi na uhalali wa zoezi hilo la kidemokrasia.
Haya yanajiri wiki chache baada ya Baraza la Katiba la Senegal kuchapisha orodha ya mwisho ya wagombea 20 wa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika nchini humo Februari 25 ambayo haikuwajumuisha kiongozi wa upinzani aliyefungwa Ousmane Sonko, na Karim Wade, mtoto wa rais wa zamani wa nchi hiyo Abdoulaye Wade.
Walioorodheshwa katika orodha hiyo ya wagombea wa kiti cha urais ni pamoja na Waziri Mkuu Amadou Ba, aliyeteuliwa na Rais wa sasa Macky Sall kuwa mrithi wake.
Rais Sall, aliyechaguliwa mwaka wa 2012 kuongoza Senegal kwa kipindi cha miaka saba na akachaguliwa tena mwaka wa 2019 kwa ajili ya kipindi cha miaka mitano, alitangaza mapema mwezi Julai mwaka jana kwamba hatagombea tena urais kuwania muhula wa tatu.
Kuakhirishwa uchaguzi wa rais nchini Senegal, iwapo muswada huo utapasishwa na kuwa sheria, litakuwa tukio la kipekee katika nchi ambayo imefanya chaguzi nne na kushuhudia makabidhiano ya madaraka kwa amani tokea ipate uhuru kutoka kwa Mkoloni Mfaransa mwaka 1960.