Serikali ya Libya: Wanamgambo kuondoka Tripoli baada ya kufikiwa makubaliano
(last modified Fri, 23 Feb 2024 03:30:54 GMT )
Feb 23, 2024 03:30 UTC
  • Serikali ya Libya: Wanamgambo kuondoka Tripoli baada ya kufikiwa makubaliano

Makundi ya wanamgambo waliojizatiti kwa silaha na ambayo yamekuwa yakidhibiti Tripoli yamekubali kuondoka katika mji mkuu huo wa Libya.

Hayo yamesemwa na Imad Trabelsi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikal ya Libya inayotambuliwa kimataifa na kueleza kuwa, makundi hayo ya wabeba silaha yameafiki suala la kuondoka Tripoli baada ya kufikiwa makubaliano.

Trabelsi amewaambia waandishi wa habari kuwa, mikoba ya wanamgambo hao waliokuwa wameudhibiti mji mkuu wa Libya itachukuliwa na polisi wa dharura, maafisa wa jiji na wapelelezi wa jinai.

Kwa mujibu wa mapatano hayo, makundi matano ya wanamgambo yanatakiwa yawe yameondoka Tripoli kufikia mwishoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani (Aprili 9).

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya ameongeza kuwa, "Tokea sasa, sehemu ya wanamgambo hao ni makao makuu yao. Serikali ya Libya itawatumia tu katika mazingira maalumu, na tena kwa shughuli maalumu."

Wanamgambo Tripoli

Haya yanajiri siku chache baada ya Abdoulaye Bathily, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa umoja huo nchini humo UNSMIL, kuwataka viongozi wa Libya kuzingatia maslahi ya taifa ili kujenga Libya yenye nguvu, umoja, utulivu na mshikamano.

Mapinduzi ya Februari 17 mwaka 2011 yaliung'oa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Lakini tangu wakati huo, Libya imetumbukia kwenye machafuko ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe huku nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ikijitahidi kufanya mabadiliko ya kidemokrasia.

Libya ilishindwa kufanya uchaguzi mkuu mwezi Disemba 2021 kama ulivyopangwa awali kutokana na kutoelewana vyama vya Libya kuhusu sheria za uchaguzi.