Feb 24, 2024 10:43 UTC
  • Deni la taifa la Tanzania lapanda kwa asilimia 17 hadi dola bilioni 34

Deni la Taifa la Tanzania liliongezeka kwa zaidi ya Tsh12 trilioni ( Dola bilioni 4.71), au asilimia 17, hadi kufikia Tsh87.47 trilioni ( Dola bilioni 34.3 bilioni) kufikia Desemba 2023.

Kwa mujibu wa gazeti la The East African, Kamati ya Bunge ya Bajeti, katika Ripoti yake ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali iliyohusu Februari 2023 hadi Januari 2024, ilisema kuwa deni la serikali lilipanda kwa kasi kutoka Tsh80.33 trilioni (dola bilioni 31) Juni 2023.

Mnamo Desemba 2022, deni la taifa lilikuwa Tsh74.75 trilioni ($29.31 bilioni)Wabunge wamesema sasa, deni la taifa linajumuisha takriban asilimia 35 ya Pato la Taifa la Tanzania kwa mwaka.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Daniel Sillo alisema wiki hii mjini Dodoma kuwa ongezeko la deni la Serikali limechangiwa na ongezeko la fedha za miradi yake ya kimkakati kama vile barabara, reli, viwanja vya ndege, maji na usambazaji wa umeme.

Pesa zingine zilielekezwa kwenye huduma za kijamii, hasa huduma za elimu na afya, na miradi ya ya kilimoSillo alisema deni la nje limeongezeka kutokana na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha pamoja na riba ya mikopo kulingana na mabadiliko ya hali ya soko.

Bunge la Tanzania

Deni la nje ni Tsh56.79 trilioni ( dola bilioni 22 bilioni) wakati deni la ndani ni Tsh30.67 trilioni ( dola bilioni12 bilioni), ripoti ya kamati ilisema.

Ripoti ya wabunge hao ilisema kuwa asilimia 28 ya deni la nje lina riba inayobadilika kulingana na soko huku asilimia 71.7 ikiwa na riba isiyobadilika.

Kamati hiyo ya bunge iliishauri serikali kuongeza makusanyo ya mapato na kujadiliana na wakopeshaji wa kibiashara na taasisi nyingine zenye riba kubwa ili kuipunguza.

Hayo yanaripotiwa wakati ambao  Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 za Afrika ambazo zitakuwa na uchumi unaokuwa kasi kiuchumi duniani mwaka 2024. Hayo ni kulingana na ripoti ya hivi punde ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Uchumi wa Tanzania mwaka huu utastawi kwa asilimi 6.1% na hivyo kuifanya kuwa kati ya 20 zinazokua kwa kasi kiuchumi duniani mwaka 2024.