Afrika Kusini yaitaka ICJ ichukue hatua za dharura dhidi ya Israel
(last modified Thu, 07 Mar 2024 03:17:46 GMT )
Mar 07, 2024 03:17 UTC
  • Afrika Kusini yaitaka ICJ ichukue hatua za dharura dhidi ya Israel

Afrika Kusini imewasilisha ombi la dharura katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ikiitaka korti hiyo ya Umoja wa Mataifa ichukue hatua zaidi za dharura dhidi ya Israel, ikisisitiza kuwa utawala huo wa Kizayuni umeendelea kupuuza amri iliyotolewa na chombo hicho cha sheria.

Vincent Magwenya, Msemaji wa Rais wa Afrika Kusini ameiambia kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar kuwa, lengo la nchi hiyo ya Kiafrika kuwasilisha ombi jipya katika mahakama ya ICJ ni kuzuia baa la njaa linaloukodolea macho Ukanda wa Gaza, sanjari na kutaka kudhaminiwa usalama na afya wakazi milioni 2.3 wa eneo hilo lililozingirwa.

Katika faili hilo lililowasilishwa jana, Afrika Kusini imeiasa ICJ ichukue hatua za dharura za kuzuia janga kubwa la kibinadamu huko Gaza, ikisisitiza kuwa Wapalestina wa Gaza wako katika hatari kubwa ya kufa njaa.

Taarifa ya Msemaji wa Rais wa Afrika Kusini imeeleza kuwa: Watu wa Gaza hawawezi kuvumilia tena. Tishio la baa la njaa sasa lipo wazi. ICJ inapasa kuchukua hatua sasa hivi ili kuzuia janga kubwa la kibinadamu kwa kuhakikisha kuwa haki za msingi zilizoainishwa kwenye Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari zinalindwa.

Afrika Kusini imeiambia ICJ kuwa, watoto zaidi ya milioni moja wa Gaza wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na makali ya njaa, na kwamba chombo hicho cha UN kinapasa kuchukua hatua zaidi kuizuia Israel kupanua operesheni zake za kijeshi katika ukanda huo ulio chini ya mzingiro wa kibaguzi.

Watoto wa Gaza wenye utapiamlo katika hatari ya kufa njaa

Afrika Kusini imekuwa mstari wa mbele kupinga na kulaani vita vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7. Mwaka jana, nchi hiyo ilifungua kesi katika Mahakama ya ICJ huko The Hague, Uholanzi ikiituhumu Israel kwa mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza. 

Serikali ya Afrika Kusini imesisitiza kuhusu kutekelezwa hukumu ya ICJ dhidi ya utawala wa Kizayuni. Mahakama ya ICJ baada ya kuchunguza mashtaka yaliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni, Januari 26 mwaka huu, ilisisitiza kuhusu ulazima wa kuchukuliwa hatua za dharura huko Ukanda wa Gaza, na kutangaza katika hukumu yake kuwa Israel inayotekeleza mauaji ya kizazi inapasa kuchukua hatua zinazohitajika ili kuzuia uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya kundi la wanadamu.