Mar 08, 2024 07:22 UTC
  • Mali, Niger na Burkina Faso zaunda muungano wa kijeshi

Mali, Niger na Burkina Faso zimetangaza habari ya kuunda kikosi cha pamoja cha jeshi kitakachosaidia kukabiliana na utovu wa usalama uliosababishwa na harakati za makundi ya kigaidi katika nchi hizo za Afrika Magharibi.

Shirika Rasmi la Habari la Niger lilitangaza habari hiyo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, wakuu wa majeshi ya nchi hizo tatu waliafikiana juu ya kuunda jeshi la pamoja la nchi hizo za Sahel baada ya kufanya mkutano jijini Niamey.

Shirika la habari la Anadolu limetangaza habari hiyo na kueleza kuwa, Mali, Niger na Burkina Faso zimechukua hatua hiyo, kwa shabaha ya kuimarisha usalama wao chini ya Muungano wa Nchi za Sahel (AES).

Idadi ya wahanga wa ugaidi nchini Mali, Burkina Faso na Niger iliongezeka mara tano baada ya 2016, na watu 4,000 waliuawa na magaidi na watu wenye itikadi kali katika nchi hizi mwaka 2019.

Ramani inayoonyesha nchi za Sahel zikiwemo Niger, Burkina Faso na Mali

Viongozi wa kijeshi wa nchi hizo wanaungwa mkono na wananchi kutokana na kufanikiwa kwao kuwatimua askari wa madola ya kibeberu ya Magharibi kama vile Ufaransa kwenye nchi hizo.

Januari mwaka huu, Niger, Mali na Burkina Faso zilitangaza kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS).

Hata hivyo jumuiya hiyo ya kikanda imeanza kuchukua hatua za kuzishawishi nchi hizo muhimu za eneo la Sahel zirejee kwenye muungano huo kwa kuziondolea vikwazo. 

Tags