Angola: Tshisekedi aafiki kukutana na Kagame kujadili machafuko mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i109412-angola_tshisekedi_aafiki_kukutana_na_kagame_kujadili_machafuko_mashariki_mwa_kongo
Viongozi wa nchi mbili zenye mvutano yaani Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanatazamiwa kukutana ili kujadili hali ya machafuko katika maeneo ya mashariki mwa Kongo ambayo Kigali imekuwa ikituhumiwa kuyachochea.
(last modified 2024-03-12T04:23:24+00:00 )
Mar 12, 2024 04:23 UTC
  • Angola: Tshisekedi aafiki kukutana na Kagame kujadili machafuko mashariki mwa Kongo

Viongozi wa nchi mbili zenye mvutano yaani Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanatazamiwa kukutana ili kujadili hali ya machafuko katika maeneo ya mashariki mwa Kongo ambayo Kigali imekuwa ikituhumiwa kuyachochea.

Mapigano kati ya waasi wa Kitutsi M23 na wanajeshi wa serikali ya Kongo DR yamewalazimisha watu zaidi ya 100,000 kukimbia makazi yao. 

Shirika la habari la Xinhua limeripoti kuwa, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, yuko tayari kukutana na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi kujadili mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC, huku tarehe na eneo na mkutano huo vikiwa bado havijawekwa wazi. 

Utayarifu wa kufanya mazungumzo ulielezwa wakati wa ziara ya Kagame huko Luanda, mji mkuu wa Angola jana Jumatatu, ambapo alikutana na Rais wa nchi hiyo, Joao Lourenco. Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Tete Antonio alitangaza taarifa hii baada ya mkutano kati ya viongozi hao wawili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola ameeleza kuwa, nchi mbili za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimekubaliana kimsingi kufanya mkutano ambapo mawaziri wa pande mbili watakutana ili kufanikisha lengo hilo. 

Ziara ya jana ya Kagame huko Angola imefuatia ile ya mwenzake wa Kongo nchini humo mwezi Februari mwaka huu. Wakati huo ilielezwa kuwa Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amekubali kukutana ana kwa ana na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame.  

Rais wa Angola ambaye anahudumu kama msuluhishi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika (AU) amekuwa akifanya juhudi za kuwakutanisha viongozi hao wawili ingawa tarehe mahsusi ya kukutana ana kwa ana haijatangazwa hadi sasa.

Rais Joao Laurenco wa Angola 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaituhumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi wa M23; tuhuma ambazo zimekanushwa na serikali ya Kigali na kundi hilo la waasi.