Magaidi 16 wa kundi la Boko Haram wauawa na jeshi la Nigeria
Vyombo vya usalama vya Nigeria vimetangaza kuwa, magaidi 16 wa kundi la Boko Haram wameuawa na jeshi kaskazini mwa nchi hiyo.
Msemaji wa jeshi la Nigeria Kanali Sani Kukasheka Usman ametangaza kuwa, wanachama hao 16 wa kundi la Boko Haram wameuawa baada ya kujiri mapigano kati yao na jeshi katika maeneo yenye machafuko ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Aidha amesema kuwa, wanajeshi wa serikali walioko katika jimbo la Borno walifyatuliana risasi kwa masaa kadhaa na wanachama hao wa Boko Haram.
Licha ya serikali ya Nigeria kutangaza kuwa imebadilisha mbinu za kupambana na Boko Haram, lakini inaonekana kuwa, kukabiliana na wanamgambo hao bado ni changamoto kubwa inayoikabili serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo.
Itakumbukwa kuwa, mwezi Machi mwaka huu, Benki ya Dunia ilitangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram la nchini Nigeria hadi sasa wameua watu zaidi ya 20 elfu na kusababisha hasara ya dola bilioni 5.9 katika jimbo la Borno. Aidha ripoti hiyo ilisema zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa kundi hilo la Boko Haram.