Kikao cha wakuu wa jeshi la Eneo la Ziwa Chad huko Niger
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11005-kikao_cha_wakuu_wa_jeshi_la_eneo_la_ziwa_chad_huko_niger
Wakuu wa kijeshi wa nchi za Niger, Chad, Cameroon na Nigeria wamekutana na kufanya mazungumzo huko Diffa kusini mashariki mwa Niger katika fremu ya mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 11, 2016 02:43 UTC
  • Kikao cha wakuu wa jeshi la  Eneo la Ziwa Chad huko Niger

Wakuu wa kijeshi wa nchi za Niger, Chad, Cameroon na Nigeria wamekutana na kufanya mazungumzo huko Diffa kusini mashariki mwa Niger katika fremu ya mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram.

Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kuwasilisha mitazamo mbalimbali na namna ya kuratibu oparesheni za kupambana na wanamgambo wa Boko Haram katika eneo. Aidha ajenda nyingine kuu ya kikao cha Diffa ilikuwa ni kuandaa mipango na ripoti tangu kuanza mashambulizi ya kikosi cha pamoja cha nchi kadhaa za Kiafrika dhidi ya kundi hilo la kigaidi. Lamidi Adeosun Jenerali wa Nigeria ambaye ni kamanda wa kikosi cha pamoja cha nchi hizo za Kiafrika za eneo la Ziwa Chad ameshiriki pia katika kikao hicho.

Kikao hicho ni mkutano wa kwanza kuwahi kufanyika baada ya mashambulizi makubwa ya umwagaji damu yaliyofanywa na Boko Haram mwezi mmoja uliopita katika eneo la Bosso huko Niger katika mpaka wa pamona na Nigeria, ambapo wanajeshi 26 wa Nigeria waliuawa.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kwa mara kadhaa sasa limezidisha mashambulizi yake katika nchi nyingine za eneo zikiwemo Niger, Cameroon na Chad pia, mbali na kutekeleza hujuma za kigaidi huko Nigeria.

Raia wasiopungua saba waliuawa siku ya Jumamosi katika mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Boko Haram katika jimbo la Borno kaskazini mwa Nigeria na kusababisha hasara kubwa kwa makazi ya raia wa eneo hilo.

Duru za usalama za Cameroon zimeripoti kuwa raia wasiopungua wawili waliuawa Ijumaa iliyopita katika shambulio la Boko Haram katika eneo la Goulouzivin kaskazini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Nigeria.

Aidha watu wengne 11 waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa kwenye mripuko uliotokea Jumatano usiku karibu na msikiti mmoja katika kijiji cha Djakana kaskazini mwa Cameroon na karibu na mpaka wa Nigeria.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa ngome za wanamgambo wa Boko Haram zimedhoofika kufuatia mafanikio iliyopata jeshi la Nigeria na vikosi vya nchi nyingine za eneo. Ngome nyingi za Boko Haram zilishambuliwa katiika oparesheni za kijeshi mwaka uliopita na kuwafanya wanamgambo wa kundi hilo kuyakimbia baadhi ya maeneo waliyokuwa wakiyashikilia.

Nigeria na Chad, Niger, Cameroon na Benin mwaka jana zilikubaliana kuunda jeshi lenye wanajeshi 8700, polisi na raia kwa ajili ya kuendesha vita vikubwa dhidi ya Boko Haram kwa kuungwa mkono na Umoja wa Afrika. Hata hivyo licha ya nchi za eneo kusisitiza kuendeshwa kwa utaratibu mapambano dhidi ya kundi hilo, weledi wa mambo wanasema kuwa hadi sasa nchi hizo hazijachukua hatua yoyote ya kivitendo katika uwanja huo.

Hata kama eneo kuu la kujiri hakarati za kundi hilo ni huko Nigeria na Rais Buhari wa nchi hiyo hadi sasa akiwa ametoa ahadi mara kadhaa za kupambana vikali ili kulitokomeza kundi la Boko Haram, lakini hatua zilizochukuliwa hadi sasa dhidi ya magaidi wa kundi hilo hazitoshi. Rais wa Nigeria hivi karibuni alimteuwa Muhammad Othman kuwa Mkuu wa Idara ya Intelijinsia na Ulinzi ya nchi hiyo.

Wachambuzi wa mambo wa kieneo wameitathmini hatua hiyo ya Rais Buhari kuwa imetekelezwa kwa lengo la kubadili siasa jumla za Nigeria na vile vile kutilia mkazo zaidi stratejia ya ukusanyaji taarifa kama njia pekee ya kukabiliana na vitisho vya kiusalama vya Boko Haram. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini pia kwamba kwa kuzingatia kushtadi mashambulizi ya Boko Haram; kutekelezwa oparesheni za ukusanyji taarifa na kushirikiana pakubwa nchi za eneo katika uwanja huo kunaweza kwa kiasi kikubwa kuandaa uwanja wa kuzimwa mashambulizi ya Boko Haram. Hata kama kufanyika vikao hivyo vya kieneo kwa kiasi fulani kunaweza kutathminiwa kuwa ni hatua moja mbele katika kuandaa mipango ya kuendesha vita dhidi ya Boko Haram, lakini vikao hivyo vitaweza kupata mafanikio ya kweli iwapo tu nchi za eneo zitachukua hatua ya kivitendo ya kushirikiana bega kwa bega katika vita dhidi ya Boko Haram kwa mujibu siasa zilizoainishwa.