Kampeni za uchaguzi zasimamishwa Zambia kutokana na machafuko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11020-kampeni_za_uchaguzi_zasimamishwa_zambia_kutokana_na_machafuko
Machafuko ya kabla ya uchaguzi mkuu nchini Zambia yamesababisha kufutiliwa mbali kampeni za uchaguzi huo katika mji mkuu Lusaka na viunga vyake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2016 02:54 UTC
  • Kampeni za uchaguzi zasimamishwa Zambia kutokana na machafuko

Machafuko ya kabla ya uchaguzi mkuu nchini Zambia yamesababisha kufutiliwa mbali kampeni za uchaguzi huo katika mji mkuu Lusaka na viunga vyake.

Tume ya Uchaguzi Zambia imesema imelazimika kusitisha kampeni hizo kutokana na kushadidi mgogoro na machafuko ya kisiasa mjini Lusaka. Taarifa ya tume hiyo imeongeza kuwa, kampeni hizo zimesimamishwa hadi Julai 18 mjini Lusaka na katika eneo la Namwala, kusini mwa mji mkuu huo.

Wakati huohuo, Kakoma Kanganja, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo amesema machafuko hayo ya kabla ya uchaguzi yalipelekea kuuawa mfuasi mmoja wa upinzani katika maandamano ya Ijumaa mjini Lusaka. Aidha ametishia kuiagiza Tume ya Uchaguzi kusitisha kampeni katika miji mingine mitatu iwapo hali ya mchafukoge itaendelea kushuhudiwa.

Hivi karibuni, Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda aliwataka wadau wa kisiasa na viongozi wa Tume ya Uchaguzi nchini kufanya mazungumzo ya kutatua matatizo hayo ya kisiasa na kusisitiza kuwa, hiyo ndio njia pekee itakayosaidia kuimarisha usalama na amani nchini humo.

Migogoro ya kisiasa nchini Zambia imeshika kasi katika hali ambayo, nchi hiyo inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa rais, bunge na madiwani uliopangwa kufanyika tarehe 11 mwezi Agosti mwaka huu.