Apr 08, 2024 12:17 UTC
  • Meli iliyozama Ziwa Tanganyika ni mali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeeleza kuwa meli inayotambulika kwa jina la MV Maman Benita, iliyozama katika eneo la Kabimba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) ni mali ya kampuni kutoka nchini humo.

TASAC imefafanua kuwa kabla ya kuzama kwa meli hiyo katika Ziwa Tanganyika, ilianza safari yake Aprili 6, 2024 saa 12 jioni ikitokea bandari ya Kigoma kuelekea Kalemie nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa imebeba jumla ya abiria 27.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, abiria hao ni pamoja na Watanzania watano, raia wa China wanne, raia wa Kongo kumi na sita, raia mmoja wa Kenya pamoja na mtoto mdogo.

Meli hiyo iliyotarajiwa kuwasili Kalemie majira ya saa nane usiku, hata hivyo haikufika, ambapo asubuhi ya Aprili 7, 2024, wavuvi walifanikiwa kumwokoa abiria mmoja mwenye asili ya China, na kisha kutoa taarifa kwa mamlaka za Serikali ya Kongo kuhusu kuzama kwa meli hiyo ya MV Maman Benita.

Baada ya kupata taarifa hiyo, zoezi la utafutaji na uokoaji lilianza mara moja ambapo hadi kufikia majira ya saa 1:00 usiku wa April 7, 2024, waathrika 17 walikuwa wameshaokolewa, kati yao ikijumuisha Wachina 2, Watanzania 3, na Wakongo 12.

Aidha, chanzo cha kuzama kwa meli bado hakijajulikana isipokuwa Nahodha wa meli hiyo ameokolewa; na timu ya wataalam tayari imekwenda eneo la tukio kwa ajili ya ufuatiliaji. Zoezi la utafutaji kuokoa abiria waliosalia linaendelea.

 

Tags