Apr 18, 2024 12:03 UTC
  • Burkina Faso yawafukuza wanadiplomasia watatu wa Ufaransa

Wizara ya Mambo ya Nje nchini Burkina Faso imewataka wanadiplomasia watatu wa Ufaransa, wakiwemo washauri wawili wa kisiasa katika ubalozi wa Ufaransa mjini Ouagadougou, kuondoka nchini humo baada ya kuwatangaza "kuwa ni watu wasiotakikana" kutokana na kile ilichokiita shughuli za uharibifu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Burkina Faso imeandika katika waraka uliotumwa kwenye ubalozi wa Ufaransa kwamba wanadiplomasia hao watatu "wamewekwa kwenye orodha ya watu wasiotakika katika ardhi ya Burkina Faso kutokana na shughuli zao za uharibifu na wametakiwa kuondoka nchini ndani ya masaa 48.” 

Vyanzo vya usalama nchini Burkina Faso vinasema, tarehe Mosi Disemba mwaka jana, wafanyakazi 4 wa serikali ya Ufaransa, ambao mamlaka ya Burkina Faso ilisema walikuwa maajenti wa ujasusi, walikamatwa nchini humo na sasa wako chini ya kizuizi cha nyumbani.

Wakati huo, chanzo cha kidiplomasia cha Ufaransa huko Ouagadougou kilisema kwamba walikuwa mafundi wa kutengeneza kompyuta, "na wameshtakiwa na kufungwa."

Katikati ya mwezi wa Septemba Burkina Faso pia iliamua kumfukuza mwambata wa kijeshi katika Ubalozi wa Ufaransa kwa madai ya kujihusisha na "shughuli za uharibifu" na kumpa muda wa wiki mbili kuondoka nchini humo.

Uhusiano kati ya Ufaransa na Burkina Faso umezorota tangu Ibrahim Traoré aingie madarakani Septemba 2022 kupitia mapinduzi ambayo yalikuwa ya pili katika kipindi cha miezi 8, huku nchi hiyo ikikomesha makubaliano ya kijeshi na Paris na kufukuza vikosi vya jeshi la Ufaransa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.