Apr 19, 2024 02:45 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu mgogoro wa kibinadamu mashariki mwa DRC

Mkuu wa kitengo cha haki za binadamu cha Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa mataifa ya dunia kuzingatia vita vinavyoendelea katika jimbo la Kivu Kaskazini la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mgogoro wa kibinadamu kwenye eneo hilo.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Turk, alitembelea kambi ya wakimbizi wa ndani, nje kidogo ya mji wa Goma ambao ndiyo makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, na kukutana kwa karibu na wananchi waliokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na waasi wa Machi 23 au kwa kifupi M23.

Amesisitizia haja ya kufanyiwa kazi mambo yanayosababisha mgogoro huo akisema: "Lazima tufanye kazi kwa bidii ili amani ipatikane."

Turk yuko katika ziara rasmi huko DRC kwa mwaliko wa serikali ya Kongo. Anatarajiwa kukutana na Rais Felix Tshisekedi na maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu, Kinshasa.

Tangu mwezi Januari, genge la M23 limezidisha mashambulizi dhidi ya raia, wanajeshi wa DRC na washirika wao, na kuteka maeneo mengine zaidi ikiwemo miji mikubwa na vijiji katika jimbo la Kivu Kaskazini. Viongozi wa Kinshasa wanailaumu Rwanda kuwa inawasaidia waasi hao wa Kitutsi.

Vita hivyo vimepelekea kuongezeka wakimbizi ambao wengi wao wamejikusanya kwenye viunga vya karibu na mji wa Goma na kuzidisha vitendo vya uhalifu na idadi kubwa ya watu walioko hatarini kuhama makazi yao.

Maeneo ya Rutshuru na Masisi kwa sasa yanakabiliwa na matokeo mabaya zaidi ya mzozo huo.