Askari wa Burundi watimuliwa CAR kutokana na jinai
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1108-askari_wa_burundi_watimuliwa_car_kutokana_na_jinai
Askari watatu wa kulinda amani wa Burundi walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati wametimuliwa baada ya kushukiwa kuwa walihusika na ukiukaji wa haki za bainadamu katika ghasia za kisiasa zinazoendelea katika nchi yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2016 12:20 UTC
  • Askari wa Burundi watimuliwa CAR kutokana na jinai

Askari watatu wa kulinda amani wa Burundi walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati wametimuliwa baada ya kushukiwa kuwa walihusika na ukiukaji wa haki za bainadamu katika ghasia za kisiasa zinazoendelea katika nchi yao.

Imebainika kuwa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA mnamo Februari 5 kiliiandikia barua Idara Kuu ya Kulinda amani ya Umoja wa Mataifa (DPKO) na kuitaarifu kuhusu uamuzi wa kuwatimua maafisa hao.

Barua hiyo ilisema Idara ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa ilibainisha wasi wasi wake kuhusu kuhusika maafisa hao katika kukiuka haki za binadamu wakati wa maandamano ya wapinzani nchini Burundi. Maafisa wa serikali ya Burundi hawajatoa taarifa yoyote kufuatia uamuzi huo. Burundi ina maafisa 1,200 wa kijeshi na polisi wanaohudumu katika vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa maeneo mbali mbali duniani. Ni jambo la kawaida kwa maafisa wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kurejeshwa makwao kutokana na vitendo vya jinai wakiwa wanahudumu kama walinda amani. Hata hivyo ni nadra kusikia maafisa wakitimuliwa kutokana na jinai walizotenda katika nchi zao. Vladimir Monteiro, msemaji wa MINUSCA amesema maafisa hao wa kulinda amani wa Burundi walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati wametimuliwa lakini hakufafanua kuhusu tuhuma dhidi yao.

Machafuko yalianza Burundi Aprili mwaka jana kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu. Nkurunziza alishinda uchaguzi huo wa mwezi Julai na hadi wakati huu nchi hiyo, hasa mji mkuu Bujumbura, umekuwa ukishuhudia machafuko na mauaji ya mara kwa mara. Maafisa wa kijeshi wa Burundi wanatuhumiwa kuhusika na jinai na ukiukaji wa haki za binadamu katika oparesheni dhidi ya wapinzani nchini humo.