Apr 19, 2024 10:22 UTC
  • Watu 391 wafariki kwa ugonjwa wa kipindupindu na homa ya dengue nchini Sudan

Jumla ya watu 391 wameripotiwa kufariki dunia kutokana na kipindupindu na homa ya dengue katika kipindi cha mwaka mmoja wa vita nchini Sudan.

Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa: "Takriban kesi 11,000 vya kipindupindu zimesajiliwa, vikiwemo vifo 325 katika majimbo 12, huku kesi za homa ya dengue zikifikia 9,000, vikiwemo vifo 66."

Haitham Mohamed Ibrahim, Waziri wa Afya wa Sudan ndiye aliyetoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari na kuongeza kuwa, licha ya kuweko vita hivyo, lakini wizara hiyo imefanikiwa kutibu watu wengi katika majimbo yaliyoathiriwa na kipindupindu na kudhibiti kuenea ugonjwa huo.

Amegusia pia juhudi za wizara yake za kutoa huduma za kimsingi za afya na kubainisha kuwa, kutoa huduma za afya katika majimbo na mikoa yote ya Sudan ni kipaumbele cha juu kwa wizara hiyo.

Kwa mujibu wa waziri huyo, takriban tani 4,000 za dawa za kuokoa maisha, zikiwemo dawa za kutiwa kwenye mishipa, figo, za kutibu saratani na zile zinazotumika katika maabara za matibabu, zimesambazwa kwenye majimbo mbalimbali ya Sudan.

Vilevile amebainisha kuwa, Wizara ya Fedha ya Sudan ilinunua vifaa vya matibabu vya dharura kwa thamani ya pauni bilioni 19 za Sudan.

Tangu vita vilipozuka kati ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tarehe 15 Aprili 2023 hadi hivi sasa, hali ya afya nchini Sudan imekuwa mbaya sana.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu inakadiri kuwa, watu 14,790 wameuawa na wengine milioni 8.2 wamelazimika kuyahama makazi yao tangu vita hivyo vianze.