Apr 19, 2024 10:22 UTC
  • Ramaphosa asisitiza kujitolea kuiunga mkono Sudan Kusini kumaliza kipindi cha mpito kwa amani

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesisitizia dhamira ya nchi yake ya kuiunga mkono Sudan Kusini ili kuhakikisha kipindi cha mpito kinamalizika kwa amani na kidemokrasia nchini humo.

Msimamo huo wa Ramaphosa umebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Bi Naledi Pandor ambaye amemnukuu rais wa nchi hiyo akisema: "Tutatoa kila msaada unaowezekana ndani ya uwezo wetu ili kuhakikisha kipindi cha mpito kinamalizika salama Sudan Kusini.

Rais Ramaphosa alitembelea Sudan Kusini Jumanne wiki hii na kupokea maelezo mafupi kutoka kwa Rais Salva Kiir Mayardit na wadau wengine kuhusu hali ya utekelezaji wa Mkataba wa Utatuzi wa Mzozo ndani ya Jamhuri ya Sudan Kusini (R-ARCSS), ambao ulitiwa saini tarehe 12 Septemba 2018

Mkataba wa R-ARCSS utakamilika tarehe 22 Februari 2025 na ni lazima utanguliwe na uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Disemba 2024.

Akiwa mjini Juba, Rais Ramaphosa alikutana na pande zinazohusika na makubaliano ya amani na kujadiliana nao maendeleo ya utekelezaji wake.

Ramaphosa alinukuliwa akisema: “Tunaporejea Afrika Kusini, tuna matumaini kwamba pande husika zitaendelea kufanya mazungumzo na kupata muafaka kuhusu masuala ambayo hayajakamilika ya utekelezaji wa mkataba huu ili watu wa Sudan Kusini wawe na matumaini ya kumalizika kwa amani na kidemokrasia, kipindi cha mpito.” 

Aliongeza kuwa, wananchi wa Sudan Kusini wanasubiri kwa hamu uchaguzi mkuu utakaotamatisha kipindi cha mpito.