Apr 20, 2024 10:41 UTC
  • Marekani itaondoa wanajeshi wake Niger kutekeleza takwa la utawala wa kijeshi

Marekani imekubali matakwa ya serikali ya Niger ya kuondoa wanajeshi wake zaidi ya 1,000 ili kuhitimisha uwepo wa kituo chake cha muda mrefu cha ndege zisizo na rubani barani Afrika.

Afisa wa Marekani ambaye amezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake amesema, naibu waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Kurt Campbell alikubali mwito huo wa kuondoa wanajeshi wa Marekani walioko Niger, katika mkutano aliofanya jana Ijumaa mjini Washington na waziri mkuu wa serikali ya kijeshi ya nchi hiyo.
 
Kwa mujibu wa afisa huyo, mazungumzo yatafanyika mnamo siku zijazo kujadili jinsi uondoaji wa askari hao utakavyofanyika.
 
Afisa huyo ameendelea kueleza kwamba licha ya kuchukuliwa hatua hiyo, uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Marekani na Niger utaendelea kuwepo.
 
Gazeti la New York Times mapema Ijumaa liliripoti kuwa, zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Marekani wataondoka nchini Niger katika kipindi cha miezi ijayo.

Mwezi uliopita, serikali ya Niger ilitangaza kuwa imebatilisha ghafla moja makubaliano ya kijeshi ambayo yaliruhusu wanajeshi na wafanyakazi wa kiraia wa Idara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon kuwepo kwenye ardhi ya nchi hiyo.

 
Niger imekuwa makao ya kambi kubwa ya anga ya Marekani katika mji wa Agadez ulioko kilomita zipatazo 920 kutoka mji mkuu Niamey, ambayo Washington imekuwa ikiitumia kwa safari za upelelezi za ndege zake zinazobeba rubani na zisizo na rubani na kwa ajili ya shughuli nyinginezo. Marekani imewekeza pia mamia ya mamilioni ya dola kwa ajili ya utoaji mafunzo kwa jeshi la Niger tangu ilipoanza operesheni zake za kijeshi nchini humo mwaka 2013.

Hatua hiyo ya kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Niger ambayo ilikuwa ikitarajiwa na kungojewa kwa muda mrefu inaashiria mafanikio mapya ya kikanda kwa Russia, ambayo imeongeza harakati zake za kujizatiti barani Afrika na kuunga mkono watawala wa kijeshi katika nchi jirani za Mali na Burkina Faso.

Mapema mwezi huu,vyombo vya habari vya serikali ya Niger viliripoti kuwa wakufunzi wa kijeshi wa Russia wamewasili nchini humo wakiwa na mfumo wa ulinzi wa anga na vifaa vingine, kufuatia mazungumzo kati ya kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdourahamane Tiani na Rais Vladimir Putin wa Russia.../