Apr 25, 2024 07:31 UTC
  • Watu wasiopungua 32 wafariki kwa janga la mafuriko nchini Kenya

Takriban watu 32 wamefariki dunia nchini Kenya na wawili hawajulikani walipo baada ya mafuriko kukumba karibu nusu ya taifa hilo la Afrika Mashariki. Watu 103,500 wanaripotiwa kuathiriwa na janga la mafuriko nchini Keya huku mvua zikiripotiwa kuendelea nchini humo.

Baadhi ya barabara katika mji mkuu wa Kenya Nairobi zilifungwa Jumatano ya jana na vitongoji kadhaa kusalia chini ya maji baada ya siku nyingine ya mvua kubwa kunyesha hiyo jana.

Kenya imesajili mvua kubwa tangu katikati ya mwezi uliopita wa Machi, lakini mvua imezidi kunyesha wiki iliyopita, na kusababisha mafuriko makubwa. Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya linasema kuwa, limefanya uokoaji zaidi ya 188 tangu kuanza mwezi Machi.

Taarifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya imesema, wafanyakazi wake wamefanikiwa kuwaokoa watu 18 katika mtaa wa Mathare 4A ambao walikuwa "wamekwama kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jana usiku jijini Nairobi."

Barabara kuu mbili za nje ya Nairobi zilishuhudia msongamano mkubwa wa magari jana Jumatano baada ya mafuriko kuzamisha sehemu zake. Mamlaka ya Barabara ya Kenya ilifunga barabara nne ambazo ziliathirika pakubwa na kuonya kuhusu mafuriko kwa zingine mbili.

 

Shirika la Reli la Kenya lilisitisha huduma za treni za abiria kote nchini.

Tunalazimika kuchukua hatua hizi za tahadhari kwa sababu usalama wa wateja wetu daima ni wa umuhimu mkubwa kwetu," amesema mmoja wa maafisa waandamizi wa Shirika la Reli nchini Kenya.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya imeonya kuhusu kuendelea kunyesha mvua nchini humo na kkutoa mwito wa kuchukuliwa tahadhari zaidi.