Apr 26, 2024 03:07 UTC
  • HRW: Jeshi la Burkina Faso limewauwa kiholela raia 223

Jeshi la Burkina Faso limewauwa kiholela raia 223, wakiwemo watoto wachanga kadhaa na watoto wengine wengi, katika mashambulizi dhidi ya vijiji viwili vinavyotuhumiwa kushirikiana na wanamgambo wenye silaha. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Human Rights Watch iliyotolewa jana Alhamisi.

Shirika la Human Rights Watch jana lilieleza kuwa mauaji hayo ya umati yalijiri tarehe 25 mwezi Februari mwaka huu katika vijiji vya Nondin na Soro kaskazini mwa Burkina Faso na kwamba watoto 56 ni miongoni mwa wahanga wa mauaji hayo ya kiholela ya jeshi la Burkina Faso. HRW imeutaka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutoa wachunguzi na kusaidia juhudi za ndani ili kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa mauaji hayo. 

Tirana Hassan Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch ameeleza kuwa mauaji hayo ya umati yaliyojiri katika vijiji vya Nondin na Soro kaskazini mwa Burkina Faso ni mauaji ya  karibuni zaidi ya raia yaliyofanywa na wanajeshi wa Burkina Faso katika operesheni zao za kukabiliana na makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha. 

Jeshi la Burkina Faso latuhumiwa kuuwa raia katika vijiji viwili 

Wanamgambo hao wenye wamekuwa wakiibua machafuko kwa kutekeleza mashambulizi mara kwa mara dhidi ya raia na dhidi ya maeneo ya serikali na hivyo na kutatiza hali ya usalama huko Burkina Faso.

Tirana ameongeza kuwa:" Msaada wa kimataifa ni muhimu ili kusaidia kufanyika uchunguzi wa kuaminika  juu ya uwezekano wa kutekelezwa jinai dhidi ya binadamu."

Mapema mwezi huu wa Aprili Shirika la habari la Associated Press lilithibitisha kujiri shambulizi la  jeshi la Burkina Faso mnamo Novemba 5 katika kijiji kingine nchini humo ambalo liliua takriban watu 70. Jeshi la Burkina Faso liliwatuhumu wanavijiji kuwa wanashirikiana na wanamgambo wanaobeba silaha na kisha liliwauwa wanavijiji hao hata watoto wachanga. 

 

Tags