UNHCR: Hali ya wakimbizi Sudan Kusini ni mbaya sana
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa hali ya raia wanaokimbia vita na mapigano ya ndani Sudan Kusini inatia wasiwasi mkubwa.
Taarifa iliyotolewa na UNHCR imesema kuwa, kila wiki wakimbizi 100 wa Sudan Kusini wanapewa makazi katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya na kwamba suala hilo limezidisha hali mbaya ya wakimbizi katika eneo hilo.
Taarifa ya UNHCR inasema kuwa, tangu mwaka 2013 hadi sasa zaidi ya raia milioni mbili wa Sudan Kusini wamelazimika kuwa wakimbizi katika maeneo mbalimbali na kwamba karibu laki saba miongoni mwao wamevuka mpaka na kuingia maeneo ya kaskazini mwa Kenya.
Taarifa ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, uhaba wa mvua na ukame mkubwa na njaa inayowasumbua wakimbizi hao ndiyo changamoto kubwa zaidi inayowakabili wakimbizi hao. Imesema vilevile wanakabiliwa na hatari ya kushambuliwa na makundi ya waasi wanapokuwa njiani wakikimbia vita na mapigano.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuwekwa vikwazo dhidi ya viongozi wa pande mbili zinazopigana nchini Sudan Kusini.
Mamia ya watu wameuawa tangu kulipoibuka mapigano mapya kati ya jeshi la serikali ya Rais Salva Kiir na wapiganaji watiifu kwa makamu wake, Riek Machar.