May 08, 2024 03:16 UTC
  • Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune
    Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune

Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, amesisitiza kwamba suala la kumbukumbu kati ya Algeria na mkoloni wa zamani, Ufaransa, "halikubali makubaliano au mazungumzo," na lazima lishughulikiwe kwa ujasiri ili kurejesha imani kati ya nchi hizo mbili.

Haya yamekuja katika ujumbe uliotolewa na Rais wa Algeria jana Jumanne, katika hafla ya Siku ya Kumbukumbu ya Kitaifa.

Katika kumbukumbu ya mauaji ya Mei 8, 1945, Tebboune amesema: "Faili la kumbukumbu halifi au kusahaulika kwa sababu ya kupita kwa miaka, na halikubali makubaliano au maelewano, litabaki kuwa kiini cha wasiwasi wetu mpaka ishughulikiwe kwa ujasiri, na kwa kuitendea haki historia.”

Kwa Waalgeria, siku hiyo inasadifiana na matukio ya umwagaji damu ambayo yalianza kwa maandamano mashariki mwa nchi, haswa katika mji wa Setif, kusherehekea ushindi wa vikosi vya Waitifaki dhidi ya Manazi, kisha yakageuka na kuwa harakati ya kudai "Algeria huru na inayojitawa" ambayo ilikandamizwa na vikosi vamizi vya Ufaransa, vilivyoua maelfu ya Waalgeria.

Tangu 2022, kamati ya pamoja ya wanahistoria 10, - (5 kutoka kila upande) - imekuwa ikifanya kazi "kuangalia kipindi hicho cha kihistoria" tangu mwanzo wa uvamizi wa Ufaransa huko Algeria mnamo 1830 hadi mwisho wa mapambano ya Uhuru mnamo 1962.

Miongoni mwa matokeo ya vikao hivyo ni pendekezo la kamati hiyo la kuweka alama "katika sehemu za kumbukumbu" nchini Ufaransa ambako walizikwa Waalgeria waliofungwa mwanzoni mwa kampeni ya ukoloni wa Ufaransa.

Waalgeriai waliouawa na Ufaransa katika mapambano ya uhuru

Mnamo 2020 Ufaransa ilikabidhi kwa Algeria mabaki ya wapiganaji 24 wa waliouawa na Wafaransa mwanzoni mwa uvamizi wa nchi hiyo huko Algeria, ambao uliendelea kwa miaka 132 kati ya 1830 na 1962. Hata hivyo, Algeria imeendelea kudai kurejeshwa kwa "mafuvu ya vichwa yaliyopo katika majumba ya makumbusho" ya Ufaransa kwa ajili ya kuzikwa upya.