Watunisia waandamana kupinga 'uingiliaji wa kigeni'
(last modified Mon, 20 May 2024 06:54:19 GMT )
May 20, 2024 06:54 UTC
  • Watunisia waandamana kupinga 'uingiliaji wa kigeni'

Wananchi wa Tunisia wamefanya maandamano kulaani na kupinga hatua ya nchi za Magharibi ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Shirika la habari la Reuters limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, wananchi wa Tunisia wanaomuunga mkono Rais Kais Saied wa nchi hiyo wamefanya maandamano hayo katika mji mkuu Tunis, kulaani uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao.

Waandamanaji hao waliokuwa wakipiga nara dhidi ya sera za uingiliaji za Wamagharibi wamesema uingiliaji wowote wa madola ya kigeni unatishia utulivu na usalama wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Wamezikosoa nchi za Magharibi kwa kuyapa mamilioni ya dola makundi ya kisiasa na kiraia ya Tunisia, ili yachochee moto wa ghasia na vurugu katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Haya yanajiri wiki moja baada ya wafuasi wa chama cha Salvation Front kinachompinga Rais Kais Saied, kuandamana katikati mwa mji mkuu, Tunis, wakitaka kusafishwa mazingira na hali ya kisiasa, kupangwa tarehe ya uchaguzi wa rais, na kutoa dhamana ya uchaguzi wa kidemokrasia na wa haki kwa wananchi.

Rais Kais Saied wa Tunisia

Waandamanaji hao pia walibeba picha za wafungwa wa kisiasa ambao wako jela tangu Februari 2023 kwa tuhuma za "kula njama dhidi ya usalama wa nchi". Miongoni mwa shakhsia walioko kizuizini nchini Tunisia ni Rashid Ghannouchi, mwanzilishi na kiongozi wa chama cha Ennahda ambaye amekuwa mtetezi shupavu wa haki za wanawake katika jamii, uchumi na taasisi za kidini.

Itakumbukwa kuwa, Julai 25, 2021 Rais Kais Saied alichukua hatua za kipekee, ikiwa ni pamoja na kuizulu serikali ya Hichem Mechichi, kulivunja Bunge na Baraza Kuu la Mahakama. Pia alibadilisha katiba ya nchi na kutwaa madaraka yote ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.