Jun 13, 2024 07:41 UTC
  • Watu 80 wakufa maji katika ajali ya boti magharibi ya DRC

Watu zaidi ya 80 wameripotiwa kuaga dunia baada ya boti iliyokuwa imewabeba kupinduka na kuzama kwenye maji ya Mto Kwa, magharibi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ren Maker, afisa wa Mamlaka ya Safari za Mitoni ya DRC alisema jana Jumatano kuwa, ajali hiyo ilihusisha boti mbili, na kwamba moja yazo ilikuwa ikielekea mji mkuu Kinshasa kabla ya injini yake kufeli.

Ameongeza kuwa, boti hiyo iligongwa na nyingine katika maji ya Mto Kwa na kusababisha ajali hiyo iliyopelekea makumi ya watu kufariki dunia.

Naye Gavana wa Mkoa wa Mai-Ndombe, Rita Bola Dula amesema kiini cha ajali hiyo ni kwa kuwa boti hiyo ilikuwa inasafiri usiku, wakati safari za usiku zimepigwa marufuku huko DRC ili kupunguza ajali.

Ajali mbaya za boti hutokea mara kwa mara katika maji ya Kongo hususan kutokana na kuwa vyombo vingi vya majini hupakia watu kupita kiasi. Nchi hiyo ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na usafiri mkubwa ni wa majini.

Boti zinavyopakia abiria na mizigo kupindukia huko DRC

Februari mwaka huu, makumi ya watu walipoteza maisha katika ajali nyingine mbaya ya boti iliyotokea katika Mto Congo, magharibi ya Kongo DR. Aidha Januari mwaka huu, watu zaidi 50 waliripotiwa kufa maji baada ya boti yao iliyoundwa kwa mbao kupinduka katika ziwa moja nchini humo.

Ofisi ya Rais wa DRC ambayo imetangaza idadi ya walioaga dunia kwenye ajali hiyo ya Jumatatu usiku kuwa ni watu 80, imetoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa wa ajali hiyo, ili kuzuia matukio kama hayo kujikariri tena. 

Tags