Jun 18, 2024 07:07 UTC
  • Genge laua watu 6 na kuteka nyara wengine 100 Nigeria

Genge la wabeba silaha limevamia kijiji kimoja huko kaskazini magharibi mwa Nigeria na kuua watu sita, mbali na kuteka nyara wengine zaidi ya 100.

Polisi nchini Nigeria jana Jumatatu walithibitisha kuwa watu zaidi ya 100 wametekwa nyara na watu wenye silaha katika uvamizi huo dhidi ya kijiji cha Tudun Doki, wilaya ya Gwadabawa katika jimbo la kaskazini magharibi la Sokoto.

Msemaji wa Polisi katika jimbo la Sokoto, Ahmed Rufai ameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, kundi hilo la wahalifu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha lilishambulia kijiji hicho Jumapili asubuhi, kabla ya Waislamu kujumuika kwa ajili ya Swala ya Iddul Adh'ha.

Abdullah Saidu, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema aghalabu ya wanakijiji waliotekwa nyara katika shambulio hilo ni wanawake, watoto wadogo na vijana.

Magaidi, majambazi na magenge ya wabeba silaha mara kwa mara hushambulia vijiji, shule na taasisi za kielemu na kuwateka nyara watu hasa wanafunzi nchini Nigeria. Mara nyingi wanadai fidia ili kuwaachilia huru mateka wao.

Mwezi uliopita, genge jingine la wabeba silaha liliwateka nyara makumi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Confluence (CUS¬TECH) katika eneo la Osara, jimbo la Kogi, kaskazini ya kati nchini Nigeria.

Kabla ya hapo pia, zaidi ya watu 100 walitekwa nyara na watu wenye silaha wakati wa uvamizi katika vijiji vitatu vilivyoko kaskazini magharibi mwa Nigeria.

 

Tags