Muungano wa waasi washambulia mkoa wa Ituri Kongo DR
Duru za kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimearifu kuwa, muungano wa makundi ya wabeba silaha umeshambulia eneo katika mkoa wa Ituri nchini humo.
Kwa mujibu wa duru hizo, miongoni mwa waasi walioshiriki katika shambulio hilo ni waasi wa Maï-Maï na wameshambulia eneo la Muchacha la mkoa huo wa Ituri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Imearifiwa kuwa, hadi sasa eneo hilo la uchimbaji wa madini, bado linadhibitiwa na wanamgambo hao. Jumuiya za kiraia za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimetangaza kuwa, zaidi ya wafanyakazi elfu 35 wanaojishughulisha na uchimbaji dhahabu wapo katika eneo hilo la Muchacha na kwamba baadhi yao wamelazimika kukimbia kutokana na kukhofia usalama wao.
Komandi ya kijeshi ya mkoa wa Ituri imesema kuwa imeanzisha operesheni ya kijeshi kwa ajili ya kuwafurusha wanamgambo hao. Eneo la mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likishuhudia machafuko kwa miaka 20 sasa huku raia wa kawaida wakiwa ndio wahanga wakuu.