Ubunifu wa miche ya migomba waleta matumaini kwa wakulima wa ndizi Tanzania
Wiki iliyopita, banda la Chuo Kikuu cha Mzumbe katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya jijini Dar es Salaam lilikuwa na msongamano wa watu.
Mashirika ya habari ya ndani na nje ya Tanzania yameangazia habari hiyo na kuripoti kuwa, wakulima wa migomba walijitokeza kwa wingi kwenye banda hilo kuona mche mpya unaostahimili magonjwa uliovumbuliwa na mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe aitwaye Gerald Cosmas Mabuto.
Maonyesho hayo ya biashara yanayoendelea chini ya kaulimbiu ya “Tanzania: Eneo lako Bora kwa Biashara na Uwekezaji” yalianza Juni 28 na yataendelea hadi Julai 13 na yamekuwa maonyesho maarufu kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania na katika nchi nyingine za Afrika.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo ya Tanzania, uzalishaji wa ndizi nchini humo umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa asilimia 5 kwa mwaka, na ulifikia tani milioni 3.2 mwaka 2022. Mkoa wa Kilimanjaro unazalisha wastani wa tani 700,000 hadi milioni 1 za ndizi kwa mwaka na hivi sasa juhudi zinaendelea kuhakikisha mkoa huo unaongeza uzalishaji wake hadi tani milioni 1.5 kwa mwaka.