Magaidi 6 wauliwa na jeshi la Niger magharibi mwa nchi
Kwa uchache magaidi sita wameuliwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya Niger karibu na kijiji cha Abdou Gangani katika mkoa wa magharibi wa nchi hiyo wa Tillabery.
Jeshi la Niger limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Operesheni hiyo ilianza Jumanne ambapo vitivo mbalimbali vya jeshi la Niger viliendesha mashambulizi dhidi ya magaidi hao na mbali na kuua magaidi hao sita, vilifanikiwa kuwatia nguvuni magaidi wengine tisa katika maeneo ya Bankilare, Torodi na Tounga na kukamata idadi kubwa ya silaha na zana za kivita zilizokuwa zinatumiwa na magaidi hao kuendeshea vitendo vyao vya kikatili.
Kijiji cha Abdou Gangani kiko katika mpaka wan chi tatu za Niger, Mali, na Burkina Faso na kimegeuzwa kuwa kituo kipya cha kuendeshea vitendo vya kigaidi na ukosefu wa usalama katika eneo la hilo. Magenge ya kigaidi yamekuwa yakitumia maeneo ya mpakani kuhatarisha usalama katika nchi za Magharibi mwa Afrika likiwemo eneo la mpakani baina ya Niger, Mali na Burkina Faso.
Magenge ya kigaidi yameongeza operesheni zao dhidi ya wananchi wa Niger baada ya kupinduliwa rais ambaye wananchi wa nchi hiyo wanasema alikuwa kibaraka mkubwa wa madola ya Magharibi na baada ya serikali mpya ya Niger kuwafukuza nchini humo askari wa madola ya kibeberu kama Marekani na Ufaransa sambamba na kuyatimua mashirika ya madola hayo ya Magharibi hasa ya Ufaransa kwa kupora utajiri mkubwa wa rasilimali ya Niger, yakiwemo madini ya urani.