Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vyaendelea kuwatesa vibaya Wasudan
Wananchi wa Sudan wanaendelea kuteseka kutokana na mgogoro mbaya zaidi wa njaa na mzozo mkubwa wa wakimbizi duniani kutokana na miezi 15 ya vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini humo.
Taarifa zinasema kuwa, wakati idadi ya watu waliouawa katika mapigano hayo ikikadiriwa kuwa ni takriban 16,000, idadi ya watu wanaopoteza maisha kutokana na kuporomoka mfumo wa huduma za afya nchini humo ni kubwa zaidi kuliko hiyo ya waliouawa katika vita.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema katika taarifa yake kuwa, tangu vita vilipoanza nchini Sudan Aprili 15, 2023 hadi hivi sasa, zaidi ya watu milioni 7.7 wamekimbia makazi yao.
IOM imebainisha kuwa, zaidi ya watu milioni 2 wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani, huku asilimia 55 wakiwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 18.
Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF limeripoti kuwa, Sudan ina idadi kubwa zaidi ya watoto waliokimbia makazi yao duniani. Inakadiriwa watoto wakimbizi huko Sudan wanaelekea kupindukia milioni 5.
Kwa mujibu wa IOM asilimia 36 ya watu waliokimbia makazi yao wanatoka Khartoum, asilimia 20 ni kutoka Darfur Kusini na asilimia 14 ni kutoka Darfur Kaskazini.
Nayo Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa, huku hali ikiendelea kuzorota kote nchini Sudan, wanawake, watoto na familia nzima wanalazimika kukimbia maeneo yao na kuacha kila kitu nyuma yao.
Naye Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus hivi karibuni alisisitiza kwamba, mtu mmoja kati ya kila watu watano nchini Sudan anahitajia msaada wa dharura wa chakula huku vita vya wenyewe kwa wenyewe vikiendelea nchini humo.