DRC: Askari wa UN kutoondoka kutokana na 'uvamizi' wa Rwanda
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) huenda kikalazimika kuakhirisha mpango wa kuwaondoa wanajeshi wake katika mkoa unaokumbwa na vita wa Kivu Kaskazini kutokana na kuwepo kwa askari wa Rwanda mashariki mwa DRC.
Waziri wa Mambo ya Nje Kongo DR, Therese Kayikwamba ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Hali ya sasa ya uwepo wa askari wa Rwanda...uvamizi wa Rwanda unafanya mpango huo (wa kuondoka askari wa UN) kuwa mgumu kutekelezwa."
Amesisitiza kuwa, pamoja na kwamba DRC inaupa umuhimu mpango wa kuondoka wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo, lakini unafaa kufanyika kwa mpangilio maalumu, iwapo mazingira yataruhusu.
Naye Bintou Keita, Mkuu wa Kikosi cha MONUSCO amesema hakuna muda maalumu wa kuondoka askari wa kikosi hicho kama walivyoombwa na Rais Felix Tshisekedi wa DRC mwezi Septemba mwaka jana.
Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kufichua katika ripoti yake kuwa, kati ya wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wanapigana bega kwa bega na waasi wa kundi la M23 huko mashariki mwa Congo DR, huku Kigali ikiongoza pakubwa oparesheni za kundi hilo.
Aidha ripoti hiyo ya UN ilisema kuwa jeshi la Uganda limetoa msaada kwa waasi wa M23 wanaoendesha harakati zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inazituhumu Uganda, Rwanda na Kenya kuwaunga mkono waasi wa M23, huku mapigano yakiongezeka na kuzusha hofu ya kutokea kwa mapigano mapya mashariki ya DRC.