Jul 16, 2024 03:14 UTC
  • Ruto: Wakfu wa US ndio unaochochea maandamano ya fujo Kenya

Rais William Ruto wa Kenya ameujia juu Wakfu wa Ford wa Marekani, akiuhusisha na vurugu zilizoshuhudiwa nchini humo wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 na jinsi utawala wa Kenya Kwanza unaendesha serikali.

Rais Ruto alisema haya jana Jumatatu akiwa katika eneobunge la Kuresoi Kusini, Kaunti ya Nakuru, ambapo ameonya kuwa, iwapo shirika hilo la kushughulikia masuala ya kijamii na lenye makao yake makuu jijini New York, Marekani litaendelea kuchochea ghasia nchini Kenya, litatimuliwa.

Rais wa Kenya amekosoa mienendo ya taasisi hiyo ya Kimarekani kwa kuhoji, “Mimi ninataka kuuliza watu wa Ford Foundation, wanatoa pesa kuchochea fujo ili wapate faida gani?"

Dakta Ruto ameeleza bayana kuwa, "Inaonekana hawana haja ya demokrasia kuwepo Kenya kwa sababu wanafadhili fujo. Tutawakashifu na kuwataka wawe wastaarabu ama waondoke.” 

Maandamano yaliyosukumwa na vijana wa kizazi cha Gen Z yalitikisa nchi hiyo ya Afrika Mashariki Juni 25, na kuishia kusababisha vifo vya watu 42 huku waandamanaji wengine wakitekwa nyara.

Maandamano ya vijana nchini Kenya

Wakati huo huo, viongozi wa kidini nchini Kenya, wakiongozwa na Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini humo (CIPK) wamewataka vijana nchini Kenya kusitisha maandamano yao yanayotarajiwa kuendelea leo Jumanne, wakihofia kudorora kwa usalama.

Wakiongozwa na Katibu Mwenezi Sheikh Mohammed Khalifa, wanasema maandamano hayo yameonyesha uzito wa kuvuruga amani ya nchi, ikiwemo kusababisha maafa na uharibifu wa mali.

CIPK inasema licha ya kuwa maandamano ni haki ya kikatiba, wanaoshiriki wanapaswa kuwa waangalifu kuhakikisha amani inadumishwa.

Tags