Jul 21, 2024 11:02 UTC
  • DRC yamuita balozi wa Uganda kujadili tuhuma za kuunga mkono M23

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imemuita balozi mdogo wa Uganda nchini humo, baada ya Umoja wa Mataifa kusema katika ripoti yake kwamba, jeshi la Uganda limewauga mkono waasi wa M23 wanaoendesha harakati zao mashariki mwa DRC.

Shirika la habari la Anadolu limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, Gracia Yamba Kazadi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemuita balozi mdogo wa Uganda nchini humo, Matata Twaha kujadili tuhuma hizo.

Balozi Twaha amekanusha madai hayo, akisisitiza kuwa Uganda imejitolea kwa dhati kushirikiana na serikali ya Kinshasa kuhakikisha kuwa usalama, amani na uthabiti vinatawala katika eneo hilo.

Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa ufichua katika ripoti yake kuwa, jeshi la Uganda limetoa msaada kwa waasi wa M23 wameshadidisha mashambulizi yao katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aidha ripoti hiyo ya UN ilidai kuwa, wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wanapigana bega kwa bega na waasi wa kundi la M23 huko mashariki mwa Congo DR, huku Kigali ikiongoza pakubwa oparesheni za kundi hilo.

Wanajeshi wa Uganda nchini DR Congo

Rais wa Rwanda Paul Kagame amekosoa ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akisema kwamba iliandikwa na wataalamu ambao wanasimulia hadithi kwa njia inayoonyesha kwamba hawana uzoefu katika faili hilo.

Mapigano makali kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali ya Kongo likishirikiana na wanajeshi wa Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani mashariki mwa DRC.

Tags