Maporomoko ya udongo yauwa watu wasiopungua 229 nchini Ethiopia
Watu wasiopungua 229 wamepoteza maisha katika maporomoko ya udongo yaliyoikumba Ethiopia baada ya mvua kubwa kunyesha nchini humo.
Watoto wadogo na akina mama wajawazito ni miongoni mwa wahanga wa maporomoko ya udongo yaliyotokea katika wilaya ya Kencho Shacha Gozdi ya kusini mwa Ethiopia.
Idadi ya waliofariki dunia imeongezeka kutoka watu 55 mwishoni mwa Jumatatu hadi 229 siku ya Jumanne huku zoezi la kuwasaka walionusurika likiendelea katika eneo hilo. Haya yameelezwa na Kassahun Abayneh, mkuu wa Ofisi ya Mawasiliano ya Kanda ya Gofa palipotokea maporomoko ya udongo.
Aghalabu ya wahanga wamefukiwa katika maporomoko ya udongo yaliyotokea juzi Jumatatu huko Ethiopia. Markos Melese Mkurugenzi wa Wakala wa Kukabiliana na Maafa katika Kanda ya Gofa amesema kuwa, hadi sasa watu wengi hawajulikani walipo miongoni mwa kundi hilo lililofukiwa na matope wakati wakijaribu kuwanusuru watu.
Maporomoko ya ardhi ni kawaida kutokea wakati wa msimu wa mvua nchini Ethiopia, ambao umeanza mwezi huu wa Julai na unatarajiwa kuendelea hadi katikati ya Septemba.