Eneo la mashariki mwa DRC laendelea kuteseka kwa wimbi jipya la mahambulizi ya waasi wa ADF, M23
Wimbi la mashambulizi mapya ya waasi wa ADF na M23 linaedelea kuwatesa wananchi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) huku mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na waasi wa makundi hayo mawili yakiendelea.
Huko Cantine, kijiji kilichoko mashariki mwa Mkoa wa Kivu Kaskazini, wanakijiji wapatao 100 waliuawa mapema mwezi Juni na waasi wa ADF. Baada ya mauaji hayo, jeshi la DRC liliahidi kuongeza vita dhidi ya ADF.
Jacques Ychaligonza Nduru, naibu mkuu wa majeshi ya DRC alisema: "Changamoto ni nyingi kwa wanajeshi wetu, lakini tuna ujumbe mmoja tu kwa watu hawa kwamba tutashinda vita hivi."
Genge la waasi la ADF lilianzishwa katika miaka ya 1990 na makundi kadhaa ya wapinzani wa Uganda. Lilishindwa na jeshi la Uganda, lakini wanachama wake waliobakia walikimbilia maeneo ya mashariki mwa DRC na wanafanya mashambulizi ya uasi hadi hivi sasa.
Tangu mwishoni mwa 2021, wanajeshi wa Uganda na Kongo wameanzisha operesheni ya pamoja ya kupambana na waasi hao wa ADF huko mashariki mwa DRC.
Gengee jingine la waasi huko mashariki mwa DRC ni lile la waasi wa M23, ambao viongozi wa DRC wanaishhutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono. Waasi hao nao kama wale wa ADF hivi sasa wameshadidisha mashambulizi yao mashariki mwa DRC na wameteka miji kadhaa tangu mwezi Juni. Wahanga wakubwa wa vitendo hivyo vya uasi ni wananchi wa kawaida hasa wanawake na watoto wadogo.