Aug 06, 2024 11:38 UTC
  • HRW: Wanajeshi wa Chad walihusika na vifo vya wafungwa wa maandamano ya 2022

Ripoti iliyotolewa leo Jumanne na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) imesema jeshi la Chad lilihusika na vifo vya wafungwa kadhaa waliokamatwa kufuatia maandamano ya Oktoba 2022.

Takriban watu wanne walipoteza maisha wakiwa njiani kuelekea gereza la Koro Toro na wengine sita walifia gerezani; na haijabainika mtu mwingine alifia wapi. Kundi hilo limesema katika ripoti yake kuwa idadi halisi ya watu waliouawa huenda ikawa kubwa zaidi.

Wakati huo, vikosi vya usalama katika taifa hilo la Afrika ya Kati, vilifyatua risasi za moto na kuuwa takriban watu 60 katika maandamano ya kupinga suala la kurefushwa utawala wa kiongozi wa muda, Mahamat Deby Itno kwa kipindi cha miaka miwili. Machafuko hayo hayakuwa ya kawaida nchini Chad, ambayo ilishuhudia upinzani mdogo wa umma wakati wa utawala wa babake, Deby Itno, ambaye alitawala nchi kwa zaidi ya miongo mitatu hadi alipouawa mwaka 2021.

Mamia ya watu walikamatwa na kupelekwa gereza la Koro Toro, umbali wa karibuu kilomita 600 kutoka mji mkuu, N'djamena.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa wito kwa mamlaka ya Chad, Umoja wa Afrika na mashirika ya Umoja wa Mataifa kuchunguza kile lilichokiita kuzuiliwa kinyume cha sheria, kutendewa vibaya gerezani, na vifo vya mahabusu.

Mfungwa wa zamani, ambaye jina lake halikutajwa, aliyenukuliwa katika ripoti hiyo amesema: "Miili ya waliouawa ilitupwa nje ya lori."