Mapigano makali yajiri baina ya wanajeshi na waasi Kivu Kaskazini
Mapigano makali yameripotiwa kujiri baina ya wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi huko Kivu Kaskazini.
Vyuombo vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimetangaza kuwa, kufuatia mapigano hayo kijiji cha Bingi huko Lubero katika jimbo la Kivu Kaskazini kimebakia kitupu baada ya wakazi wake kuyakimbia makazi yao.
Raia hao wamelazimika kuyakimbia makazi yao baada ya mapigano hayo kudumu kwa muda wa siku tatu.
Kwa mujibu wa duru za kiusalama mapigano hayo ni kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa Mai-Mai.
Raia waliokimbia makazi yao wameenda kuomba hifadhi katika maeneo mengine ya Kivu Kaskazini.
Hata hivyo hadi sasa hakuna taarifa za uhakika kuhusiana na idadi ya watu waliopoteza maisha yao kufuatia mapigano hayo..
Mapigano hayo yamepelekea kuzuka wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia ambao wamekuwa wakikimbia makazi yao ili kusalimisha maisha yao.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa likishuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Ukosefu wa usalama katika maeneo hayo umepelekea raia wengi walazimike kuyakimbia makazi yao na hivyo kuwa wakimbizi.