Baada ya wanajeshi 200, sasa Rais wa Rwanda awastaafisha kwa nguvu zaidi ya wanajeshi 1,000 wengine
(last modified Sat, 31 Aug 2024 13:03:18 GMT )
Aug 31, 2024 13:03 UTC
  • Baada ya wanajeshi 200, sasa Rais wa Rwanda awastaafisha kwa nguvu zaidi ya wanajeshi 1,000 wengine

Rais Paul Kagame wa Rwanda ameidhinisha kustaafu zaidi ya wanajeshi 1,000 kutoka jeshini, wakiwemo majenerali watano, ikiwa ni siku moja baada ya kuwafuta kazi wanajeshi wengine zaidi ya 200 wakiwemo wa ngazi za juu.

Jeshi la Rwanda limetoa taarifa hiyo leo Jumamosi na kuongeza kuwa, waliotakiwa kustaafu ni pamoja na Mkuu wa zamani wa Majeshi, Jenerali Jean Bosco Kazura pamoja na mabrigedia jenerali wanne, maafisa wakuu 170, na askari 992 wa vyeo mbalimbali waliofikia umri wa kustaafu au ambao mikataba yao ya utumishi imekamilika.

Majenerali na maafisa wakuu wanaostaafu wamekuwa wakihudumu jeshini tangu wakati wa vita vya ukombozi vya Rwanda miaka ya tisini.

Jenerali Kazura alikuwa mkuu wa wafanyakazi wa ulinzi wa Jeshi la Rwanda (RDF) kuanzia mwezi Novemba 2019 hadi Juni 2023.

Jenerali Kazura aliwahi pia kuwa naibu kamanda wa kikosi cha Umoja wa Afrika huko Darfur, Sudan, na kamanda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA).

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Kagame kuwafuta kazi askari zaidi ya 200 kutoka jeshini, wakiwemo maafisa waandamizi 20 kutokana na utovu wa nidhamu, rushwa na ukiukaji wa maadili ya jeshi.

Msemaji wa jeshi la Rwanda, Brigedia Jenerali Ronald Rwivanga aliwaambia waaandishi wa habari jana Ijumaa kwamba: "RDF itaendelea kuwa imara katika sera yake ya kutovumilia rushwa, utovu wa nidhamu na utovu wa madili."