Sep 01, 2024 06:44 UTC
  • Waziri Mkuu wa Senegal ataka kutengwa, kususiwa Israel

Waziri Mkuu wa Senegal, Ousmane Sonko ameziasa nchi za Kiislamu kuususia utawala wa Israel na kuzidisha mashinikizo ya kulitenga dola hilo la Kizayuni.

Sonko amesema hayo wakati akishiriki maandamano mapya ya Wasenegal ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina wanaotaabika kutokana na athari za vita katika Ukanda wa Gaza.

Kiongozi huyo wa Senegal amemtaja Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kama mtu anayefadhilisha kuponda maelfu ya miili chini ya miguu yake ili kuepuka kukabiliwa na mkono wa sheria.

Sonko ametoa wito wa kuwepo mshikamano zaidi miongoni mwa nchi za Kiislamu ili kuiunga mkono Palestina na kusisitiza kuwa, "Lazima tuwalete pamoja wale wote wanaochukizwa na dhulma hii, tufanye kazi kuelekea suluhisho la kisiasa ambalo ni suluhisho la kulitenga dola la Israel."

Waziri Mkuu wa Senegal amesema maandamano hayo yanashinikiza kukomeshwa ukatili ulioidhinishwa na baadhi ya nchi za Magharibi dhidi ya Wapalestina na kuongeza kuwa, "kulaani pekee hakutoshi; Senegal imedhamiria kuchukua hatua madhubuti zaidi."

Wananchi wa Senegal wamekuwa wakiandamana mara kwa mara wakitoa wito kwa seriikali yao kukata uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.

Tags