Mali: Silaha za Magharibi zinaimarisha ugaidi barani Afrika
(last modified Sun, 01 Sep 2024 07:21:45 GMT )
Sep 01, 2024 07:21 UTC
  • Mali: Silaha za Magharibi zinaimarisha ugaidi barani Afrika

Mwakilishi wa Kudumu wa Mali katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, sehemu kubwa ya silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi kwa Ukraine zinahamishiwa katika eneo la Sahel barani Afrika na kushadidisha harakati za ugaidi barani humo.

Issa Konfourou ameeleza kwamba, ataendelea kuifichulia dunia wasiwasi wa nchi za eneo la Sahel kuhusu athari za silaha zinazotolewa na Magharibi kwa usalama wa Afrika, kwa sababu ilithibiti kuwa aghalabu ya silaha zilizotumwa Ukraine zinatumika kueneza ugaidi katika sehemu mbalimbali za Afrika.

Tovuti ya habari ya Iran Press imeandika habari hiyo na kueleza kuwa, kuibuliwa suala hilo na duru na shakhsia tofauti akiwemo mwakilishi wa Mali katika Umoja wa Mataifa kunaonyesha kuwa, nchi za Magharibi zinafuatilia malengo yenye pande nyingi ambayo muhimu zaidi ni kuchangia ukuaji wa sekta yao ya kijeshi na kuyapa nguvu makundi ya kigaidi.

Hivi karibuni, Burkina Faso, Mali na Niger ziliwasilisha ombi kwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zikilitaka baraza hilo lilaani waziwazi kitendo cha Ukraine cha kuunga mkono 'ugaidi wa kimataifa' hasa katika eneo la Sahel Afrika.

Katika barua ya pamoja, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo tatu walisema kuwa, nchi zao zilishangazwa na matamshi ya kijeuri ya Andriy Yusov, msemaji wa idara ya ujasusi ya jeshi la Ukraine ambaye alikiri hadharani kuwa, nchi yake ilihusika moja kwa moja katika mashambulizi ya kiwoga, kinyama na kijinai dhidi ya wanajeshi wa Mali kati ya Julai 24 na 26 mwaka huu.

Zimelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua zinazofaa dhidi ya vitendo hivyo vya uasi vya Ukraine vinavyoimarisha magenge ya kigaidi barani Afrika.