Majaliwa: Tanzania inazidi kuimarika katika upande wa kidiplomasia
(last modified Thu, 05 Sep 2024 05:54:56 GMT )
Sep 05, 2024 05:54 UTC
  • Majaliwa: Tanzania inazidi kuimarika katika upande wa kidiplomasia

Waziri Mkuu wa Tanzania amesema kuwa, nchi hiyo inazidi kustawi kote duniani kufuatia hatua ya hivi karibuni ya kuchaguliwa raia wa nchi hiyo, Faustine Engelbert Ndugulile, kuwa, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika.

Kassim Majaliwa amesema hayo ofisini kwake, Makao Makuu ya Dodoma mbele ya Ndugulile ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika.

Amesema kuwa, serikali ya Tanzania itaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha Watanzania wengi kadiri iwezekanavyo wanapata nafasi za kazi kikanda na kimataifa.

Waziri Mkuu huyo wa Tanzania ameongeza kuwa, uongozi wa miaka mitatu wa Rais Samia Suluhu Hassan umepata mafanikio makubwa katika uwanja wa kidiplomasia, akitolea mfano kuchaguliwa Spika wa Bunge la nchi hiyo, Tulia Ackson kuwa rais wa 31 wa Muungano wa Mabunge mwezi Oktoba mwaka jana.

Kassim Majaliwa akiwa ofisini kwake dodoma katika mazungumzo na Ndugulile aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika

 

Vilevile amemhakikishia Ndugulile kwamba atapata uungaji mkono kamili wa serikali katika kipindi chake chote cha miaka mitano cha kuhudumu katika nafasi ya mkurugenzi wa kanda wa WHO, jukumu ambalo atalibeba kuanzia mwishoni mwa Februari au mwanzoni mwa mwezi Machi 2025.

Kwa upande wake, Ndugulile amemshukuru Rais wa Tanzania kwa msaada na ushawishi wake wa kidiplomasia uliomwezesha kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Ndugulile, ambaye ameshashika nyadhifa nyingi katika serikali ya Tanzania kama waziri wa habari, mawasiliano na teknolojia ya habari na naibu waziri wa afya, alichaguliwa hivi karibuni kushika nafasi hiyo wakati wa Mkutano Mkuu wa 74 wa WHO uliofanyika Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo.