Ramaphosa: Afrika ipewe kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la UN
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesisitiza kuwa Afrika inapasa kupewa uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).
Ramaphosa ameeleza bayana kuwa, ni jambo lisilokubalika kwa bara hilo lenye watu zaidi ya bilioni 1.3 kubakia bila uwakilishi katika chombo hicho muhimu cha UN.
Kiongozi huyo wa Afrika Kusini amesema kuwa, Afrika inastahili sio tu kuwa na kiti cha kudumu lakini pia kupewa haki ya kura ya turufu, ili kutobakia kwenye ushiriki wa "daraja la pili".
"Tuna uwezo, tunao ujuzi, na Afrika inahitaji kupewa nafasi yake inayostahiki katika mifumo ya Umoja wa Mataifa na miundo yake mbalimbali," ameongeza Ramaphosa.
Matamshi ya Rais wa Afrika Kusini yanakuja wiki moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kulikosoa Baraza la Usalama kwa kutokuwa na mwakilishi wa kudumu kutoka Afrika.
Mataifa yanayoendelea kwa muda mrefu yamekuwa yakidai viti vya kudumu kwenye Baraza la Usalama, chombo chenye nguvu zaidi katika Umoja wa Mataifa bila mafanikio.