Kiongozi wa upinzani Gambia ahukumiwa miaka 3 jela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11692-kiongozi_wa_upinzani_gambia_ahukumiwa_miaka_3_jela
Kiongozi wa upinzani nchini Gambia Ousainou Darboe amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 21, 2016 13:47 UTC
  • Ousainou Darboe, Kiongozi wa upinzani nchini Gambia
    Ousainou Darboe, Kiongozi wa upinzani nchini Gambia

Kiongozi wa upinzani nchini Gambia Ousainou Darboe amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.

Kiongozi huyo wa upinzani amehukumiwa kifungo hicho pamoja na watu wengine 18 baada ya kupatikana na makosa kadhaa yanayohusiana na maandamano yaliyofanywa dhidi ya serikali mwezi Aprili. Maandamano hayo yaliongozwa na Bw Darboe.

Kiongozi huyo wa upinzani alikuwa akishiriki maandamano hayo kulalamikia taarifa za kuuawa kwa mmoja wa viongozi wa chama chake, Solo Sandeng, akiwa kizuizini.

Maandamano huwa nadra sana kufanyika  nchini Gambia, ambayo imetawaliwa na Rais Yahya Jammeh tangu achukue madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi 1994.

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu na Umoja wa Mataifa yamelaani hatua hiyo. 

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Desemba, lakini viongozi wa upinzani wanasema hautakuwa huru na wa haki.

Rais Yahya Jammeh wa Gambia

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mwanzoni mwa mwezi huu Rais Yahya Jammeh wa Gambia alipiga marufuku ndoa za mabinti wenye umri wa chini ya miaka 18. Kwa mujibu wa marufuku hiyo atakayepatikana amemuoa binti mwenye umri wa chini ya miaka 18 atahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela. Aidha wazazi wa binti nao watakabiliwa na adhabu kama hiyo kwa kuruhusu binti yao mwenye umri wa chini ya miaka 18 kuolewa.