Jeshi la Nigeria: Tumeua takriban magaidi 140 katika kipindi cha wiki moja
(last modified Fri, 25 Oct 2024 10:12:56 GMT )
Oct 25, 2024 10:12 UTC
  • Jeshi la Nigeria: Tumeua takriban magaidi 140 katika kipindi cha wiki moja

Jeshi la Nigeria limetoa taarifa mpya na kutangaza kuwa, katika kipindi cha wiki moja iliyopita limefanikia kuua magaidi 140 katika operesheni maalumu zilizofanyika kwenye kona zote za nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Edward Buba, msemaji wa jeshi la Nigeria amewaambia waandishi wa habari mjini Abuja kwamba magaidi wengine 135 wametiwa mbaroni na wanajeshi katika maeneo tofauti ya operesheni hizo kwenye kipindi hicho cha wiki moja.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mateka 76 wamekombolewa kutoka mikononi mwa magaidi hao na silaha 241 za aina mbalimbali na risasi 3,254 zimekamatwa na jeshi.

Magaidi wa ISWAP wa nchini Nigeria

 

Katika sehemu moja ya matamshi yake mbele ya waandishi wa habari, Buba amesema: "Operesheni zinazoendelea za kupambana na ugaidi na kukabiliana na waasi zimewatia hasara kubwa magaidi hao. Jeshi (la Nigeria) limeamua kuendelea na operesheni hizo ili kuzuia magenge ya wahalifu yasifikie malengo yao.

Vile vile msemaji huyo wa jeshi la Nigeria amesema: "Wakati vita vikiwa vimepamba moto, askari wetu wanaendelea kutafuta utatuzi wa kiubunifu wa changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa operesheni na kukubali kubadilika kwa mujibu wa mazingira ili kuongeza mafanikio ya utendaji kazi katika nyanja zote za operesheni."

Mwezi Oktoba mwaka huu pia, jeshi la Nigeria lilitanga kuua magaidi 101 katika kipindi cha wiki moja ya operesheni zilizowalenga magaidi wa magenge ya Boko Haram, ISWAP ambalo ni tawi la genge la kigaidi la ISIS Jimbo la Afrika Magharibi pamoja na magenge mengine ya wahalifu.