Uchaguzi wa rais Benin waahirishwa hadi mwezi ujao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1180-uchaguzi_wa_rais_benin_waahirishwa_hadi_mwezi_ujao
Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini Benin ambao ulitazamiwa kufanyika mwishoi mwa mwezi huu umeahirishwa hadi mwezi ujao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 13, 2016 11:55 UTC
  • Uchaguzi wa rais Benin waahirishwa hadi mwezi ujao

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais nchini Benin ambao ulitazamiwa kufanyika mwishoi mwa mwezi huu umeahirishwa hadi mwezi ujao.

Tume ya Uchaguzi nchini humo imesema uchaguzi huo ambao ulitarajiwa kufanyika Februari 28 sasa utafanyika Machi 6. Mahakama ya Katiba nchini humo imeidhinisha kusogezwa mbele tarehe hiyo ya uchaguzi. Tume ya Uchaguzi nchini humo imesema iliomba kusogezwa mbele tarehe ya uchaguzi kutokana na sababu za kilojistiki na kwamba matayarisho ya zoezi hilo hayatakuwa yamekamilika kufikia Februari 28. Augustin Ahouanvoebla, afisa wa tume hiyo amesema kufikia Februari 11, asilimia 60 tu ya kadi za kupigia kura ndizo zilizokuwa zimechapishwa. Kadhalika upinzani nchini humo ulikua umetoa wito wa kusogezwa mbele tarehe ya uchaguzi huo kutoka na changamoto hizo za kuchapisha na kusambaza kadi za kura kwa wapiga kura wapatao milioni 4.6.

Wagombea 33 wamejitosa kwenye kinyang'anyiro cha kumrithi Rais wa sasa wa Benin, Boni Yayi ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 2006.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, Rais Yayi hawezi kuwania tena kiti chake kwa muhula wa tatu. Hata hivyo kiongozi huyo amekuwa akionekana hadharani akimuunga mkono Waziri Mkuu, Lionel Zinsou, ambaye ameteuliwa na chama tawala FCBE kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa rais.

Wengine ni Sebastien Ajavon, mfanyabiashara maarufu wa nchi hiyo na Marie Elyse Gbedo aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria wa Benin.