Wanigeria waandamana kulaani jinai za Israel Gaza na Lebanon
(last modified Sun, 27 Oct 2024 02:24:59 GMT )
Oct 27, 2024 02:24 UTC
  • Wanigeria waandamana kulaani jinai za Israel Gaza na Lebanon

Mamia ya wananchi katika Jimbo la Kano Kaskazini Magharibi mwa Nigeria wameshiriki katika maandamano ya wafuasi wa Palestina kulaani tena ukatili wa Israel dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberam wametoa wito wa kuchukuliwa hatua kali za haraka za walimwengu kukabiliana na utawala huo ghasibu wa Kizayuni.

Wafuasi hao wa Palestina wameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kusitisha jinai na mauaji ya utawala haramu wa Israel huko Gaza na Lebanon.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Israel imeendelea kupuuza miito ya walimwengu ya kusitisha vita na hivyo kulifanya eneo la gaza kukabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.

Zaidi ya Wapalestina 43,000 wameuawa shahidi tangu Israel ianzishe hujuma na mashambulio ya kijeshi dhidi ya Gaza Oktoba 2023

 

Wakati huo huo, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema, watoto Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wanakufa kwa uchungu kwa kukosa matibabu ya dharura kutokana na mamlaka za utawala wa Kizayuni wa Israel kuwazuia wasiende kupatiwa matibabu nje ya eneo hilo lililowekewa mzingiro baada ya kufungwa kivuko cha Rafah.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema maisha ya kawaida yanazidi kuwa jinamizi huko Ghaza kwa sababu kukidhi mahitaji ya msingi kama chakula ni mtihani mkubwa kwa watu wengi na kutoa mfano wa hali ilivyo katika mji wa Deir al-Balah ambako hata mkate ambao ni chakula kikuu, kupatikana ni changamoto.