Chama tawala Mauritius chakubali kushindwa katika uchaguzi Bunge
Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravind Kumar Jugnauth jana Jumatatu alikubali kushindwa muungano wake wa chama tawala katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mapema hata kabla ya kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Jumapili.
Jugnauth amekubali kushindwa muungano wa chama chake mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa: "Ni wazi kwamba Muungano wa Lepep unaelekea kushindwa kwa kiasi kikubwa."
"Nimefanya nilichoweza kwa ajili ya nchi na kwa ajili ya watu wetu. Wananchi wamechagua timu nyingine ya kuongoza nchi. Naheshimu chaguo hilo," alisema na kuongeza: "Naitakia nchi yangu na watu wake mafanikio mema."
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yalitarajiwa kutangazwa jana Jumatatu. Kiongozi wa muungano au chama chenye viti vingi Bungeni ndiye atakayeteuliwa kuwa waziri mkuu wa baadaye wa Mauritius.
Baadhi ya matokeo katika majimbo matano ya uchaguzi yalionyesha kuwa wagombea kutoka Muungano wa Change unaoongozwa na waziri mkuu wa zamani Navin Ramgoolam, walikuwa mbele sana na walikuwa wanaelekea kupata ushindi wa kishindo.
Utabiri wa timu za waangalizi wa uchaguzi zilionesha kuwa hali ingelikuwa hiyo hiyo katika majimbo yote 21 ya uchaguzi ya Mauritius.
Bunge la Mauritius lina viti 70. Wapiga kura huchagua moja kwa moja wabunge 62 wa Bunge la Taifa, huku wanane waliobakia wakiwa ni wabunge wa kuteuliwa.