Kaunti 4 za Kenya zinakabiliwa na ukame mkubwa na janga la njaa
(last modified Fri, 15 Nov 2024 11:08:44 GMT )
Nov 15, 2024 11:08 UTC
  • Kaunti 4 za Kenya zinakabiliwa na ukame mkubwa na janga la njaa

Kaunti nne ambazo ziko kwenye maeneo yanayokumbwa mno na ukame zinakabiliwa na hatari ya janga kubwa la njaa ambalo linaweza kuwatumbukiza takriban watu milioni moja katika hatari ya ukosefu wa chakula.

Katika taarifa yake ya jana Alkhamisi, Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Ukame nchini Kenya (NDMA) imesema kuwa, kaundi hizo zimetumbukia kwenye hatua ya tahadhari kubwa baada ya kupitisha muda mrefu katika hali ya kawaida.

Kaunti 23 za Kenya zinahesabiwa kuwa ziko kwenye maeneo ya ukame kwa kifupi maeneo ya ASAL.

Katika taarifa yake, Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Ukame Kenya (NDMA) imesema kuwa, hali inazidi kuwa mbaya katika kaunti nyingi za ASAL kutokana na kuchelewa msimu wa mvua za Oktoba hadi Disemba.

Kaunti 23 za Kenya ziko kwenye hatari za ukame, nne zimekaribia kwenye janga

 

Taasisi hiyo imesema pia kwamba imegundua kuweko utapiamlo uliokithiri katika kaunti zote. Imesema, watoto 479,498 wenye umri wa miezi sita hadi 59 na akina mama wajawazito na wanaonyonyesha 110,169 wana utapiamlo na wanahitaji matibabu ya haraka hivi sasa.

Kwa mujibu wa NDMA, kaunti nne za Kenya zilizoko katika awamu ya tahadhari ya ukame ni Garissa, Kilifi, Kwale na Tana River, huku kaunti zenye kesi za utapiamlo zikiwa ni pamoja na Baringo, Turkana, Kitui, Laikipia, Lamu, Makueni na Pokot Magharibi.

Shiŕika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Afŕika Mashaŕiki zimesema katika ripoti ya hivi karibuni kwamba idadi ya watu wasio na chakula katika eneo la Pembe ya Afŕika inafikia milioni 67.