Wakazi wa vijiji 5 wahama Ituri kwa kuhofia usalama wao
Duru za habari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeripoti kwamba, wakazi wa vijiji vitano vya mkoa wa Ituri, wamelazimika kuhama myumba zao kutokana na wasi wasi wa kushambuliwa na makundi ya wabeba silaha wasiojulikana.
Habari zinaeleza kuwa, wakazi wa vijiji hivyo vilivyopo katika eneo la Mambasa, mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamehama nyumba zao na kuelekea vijiji vya karibu na mkoa wa Haut-Uélé, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa duru za habari, wakazi wa vijiji hivyo wamechukua hatua hiyo baada ya kuwepo tetesi za kushambuliwa na makundi ya waasi wasiojulikana katika hali ambayo hawana ulinzi wowote.
Kufuatia hali hiyo, jeshi la serikali limetuma askari wake kwenda kuweka doria katika eneo hilo sanjari na kuwataka wanavijiji hao kurejea makwao. Komandi ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mkoa wa Ituri imesisitiza kuchukua hatua za kiusalama kwa ajili ya kudhamini usalama wa wakazi wa vijiji vya eneo hilo la Mambasa.
Ni miaka 20 sasa wakazi wa maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wamekuwa wakiishi katika hali ngumu ya vita na machafuko kutokana na kushindwa askari wa serikali na wale wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa kudhamini usalama wa wakazi wa maeneo hayo.