Familia: Afya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky sio nzuri
Familia ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, mwanachuoni na kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeeleza juu ya wasi wasi wake kuhusu hali ya kiafya ya msomi huyo wa Kiislamu.
Watu wa familia hiyo wamemwambia mwandishi wa habari wa kanali ya televisheni ya Press TV katika mji wa Zaria kuwa, afya ya Sheikh Zakzaky inazidi kuzorota, kutokana na hali ngumu anayoipitia akiwa kizuizini zaidi ya miezi saba sasa. Watu waliokutana na Sheikh Zakzaky gerezani hivi karibuni walisema jicho lake la kushoto limepofuka na kwamba juhudi za kutibu jicho lake la kulia zimekuwa na mafanikio ya kiwango fulani. Harun al-Binawi mjumbe wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, amefafanua mazingira na hali mbaya anayoipitia Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi mkuu wa harakati hiyo na kusisitiza kuwa, kitendo cha kumtia mbaroni Sheikh Zakzaky na mkewe kilichojiri katika tukio la hujuma ya kutisha ya askari wa nchi hiyo na kisha kuendelea kuwashikilia shakhsia hao katika mazingira magumu, ni uvunjwaji wa wazi wa haki za binaadamu.
Wananchi wa Nigeria wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru haraka kiongozi huyo wa Kiislamu. Itakumbukwa kuwa tarehe 12 Disemba mwaka jana vikosi vya Nigeria vilishambulia marasimu ya kidini ya Waislamu wa Kishia katika mji wa Zaria na kuwatuhumu kuwa walizuia msafara wa mkuu wa jeshi na pia kujaribu kumuua, madai ambayo yalikanushwa na Waislamu hao.
Siku iliyofuata wanajeshi hao walivamia nyumba ya Sheikh Zakzaky na kumtia nguvuni baada ya kuwapiga risasi na kuwaua wale waliojaribu kumhami kiongozi huyo akiwemo kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pamoja na watoto wake.