Mgombea urais wa chama kikuu cha upinzani Namibia: Hatutayakubali matokeo ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i119566-mgombea_urais_wa_chama_kikuu_cha_upinzani_namibia_hatutayakubali_matokeo_ya_uchaguzi
Mgombea mkuu wa urais wa upinzani nchini Namibia, Panduleni Itula, amesema chama chake hakitatambua matokeo ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa kuongezewa muda wa upigaji kura na kutawaliwa na fujo na madai ya uchakachuaji.
(last modified 2025-09-23T11:30:28+00:00 )
Dec 01, 2024 06:13 UTC
  • Mgombea urais wa chama kikuu cha upinzani Namibia: Hatutayakubali matokeo ya uchaguzi

Mgombea mkuu wa urais wa upinzani nchini Namibia, Panduleni Itula, amesema chama chake hakitatambua matokeo ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa kuongezewa muda wa upigaji kura na kutawaliwa na fujo na madai ya uchakachuaji.

Akizungumza muda mchache kabla ya kuhitimishwa muda wa upigaji kura katika siku ya mwisho ya zoezi hilo jana Jumamosi, Itula ambaye chama chake kilichomsimamisha kugombea urais cha Independent Patriots for Change (IPC) kinatarajia kuhitimisha miaka 34 ya utawala wa chama cha SWAPO, amesema bila kujali matokeo yatakavyokuwa, IPC haitayatambua matokeo ya uchaguzi huo.
 
Amesema: “utawala wa sheria umekiukwa kwa kiwango kikubwa na hatuwezi kuuita uchaguzi huu kwa njia yoyote au kipimo chochote kuwa ni uchaguzi huru, wa haki na halali".
 
Tume ya Uchaguzi ya Namibia ECN iliamua kurefusha zoezi la upigaji kura katika uchaguzi wa urais na ubunge, baada ya zoezi la siku ya awali ya uchaguzi - Jumatano - kugubikwa na hitilafu kadhaa za vifaa na za kiufundi ambazo zilisababisha misururu mirefu ya wapigakura waliobaki vituoni kwa saa nyingi, na kuwafanya hatimaye baadhi ya wananchi waamue kuondoka vituoni bila ya kupiga kura.
 
Jana Jumamosi, mamia ya watu walipanga foleni katika kituo cha pekee cha kupigia kura katika mji mkuu Windhoek, ambapo wapiga kura 2,500 walipiga kura siku ya Ijumaa.

SWAPO, ambayo imeitawala Namibia tangu nchi hiyo ipate uhuru wake kutoka kwa utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini mwaka 1990, imekabiliwa na ushindani mkubwa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Wachambuzi kadhaa walieleza wakati wa kukaribia kufanyika uchaguzi mkuu wa Namibia kwamba kuna uwezekano mkubwa wa SWAPO kuondolewa madarakani na vijana ambao ni 64% ya wapiga kura waliojiandikisha.

Inadaiwa kuwa vijana wamechoshwa na kuwepo idadi kubwa ya watu wasio na ajira, kukosekana usawa katika jamii na kuwepo kwa ufisadi; na kwa hivyo wanataka mabadiliko.../