Mwisho wa uwepo wa jeshi la Ufaransa nchini Chad
Serikali ya Chad imetangaza kukomesha makubaliano yake ya ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa na kutangaza kuwa vikosi vya jeshi la nchi hiyo vinapaswa kuondoka nchini Chad.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad, Abderaman Koulamallah, ameandika katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii kwamba: Jamhuri ya Chad inatangaza kwa nchi za dunia uamuzi wake wa kufuta makubaliano ya ushirikiano wa kiulinzi uliotiwa saini na Jamhuri ya Ufaransa.
Taarifa hiyo imetaja kukomeshwa uwepo wa kijeshi wa Ufaransa nchini Chad kama "tukio muhimu la kihistoria" na kusema kuwa: "Baada ya miongo kadhaa ya uhuru wa nchi, wakati umefika sasa kwa Chad kuwa na mamlaka kamili na kutazama upya ushirikiano wake wa kimkakati kwa mujibu wa maslahi ya taifa."

Kabla ya Chad, nchi nyingine kadhaa za Kiafrika, ikiwa ni pamoja na Mali, Niger, Gabon na Burkina Faso, zilikuwa tayari zimetangaza rasmi kukata ushirikiano wao wa kijeshi na Ufaransa. Vilevile Senegal imetangaza kuwa kambi za kijeshi za Ufaransa katika nchi hiyo ya Kiafrika zitafungwa hivi karibuni.
Ijapokuwa harakati za kupambana na ukoloni na kupigania ukombozi dhidi ya ukoloni wa Ufaransa katika nchi mbalimbali za Kiafrika kama vile Algeria katika miongo iliyopita ziliilazimisha Ufaransa kufunga virago na kutambua rasmi uhuru wa nchi hizo, lakini katika miaka ya hivi karibuni Ufaransa imerudi tena katika nchi hizo katika mfumo wa ukoloni mamboleo, kwa visingizio mbalimbali kama vile kupambana na ugaidi na kusaidia juhudi za kuimarisha amani na usalama katika nchi hizo!
Kuhusiana na suala hilo, mamia ya wanajeshi wa Ufaransa wamekuwepo katika nchi za Mali, Niger, Chad na nchi nyingine kadhaa za Kiafrika katika miaka ya hivi karibuni kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi. Hata hivyo nchi za Kiafrika hazikuridhishwa na utendaji wao. Kinyume chake, nchi za Kiafrika zinaamini kuwa utendaji wa jeshi la Ufaransa uliyaunga mkono na kuyahami makundi yenye itikadi kali kwa nia ya kudumisha vituo na kambi za Paris barani Afrika. Kupatikana ushahidi kama vile makaburi ya halaiki karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa nchini Mali, na ongezeko la mashambulizi ya kigaidi katika nchi nyingi za bara la Afrika ambazo zina idadi kubwa ya wanajeshi wa Ufaransa hususan eneo la Sahel, kulizidisha hasira za nchi za Kiafrika dhidi ya hatua za Ufaransa.
Hali hii imezidisha tena mtazamo mbaya dhidi ya Ufaransa katika nchi nyingi za Kiafrika. Mtazamo huo ulipamba moto zaidi mwanzoni mwa mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi katika nchi kadhaa za Kiafrika. Uungaji mkono wa umma kwa wanajeshi waliofanya mapinduzi na maandamano ya kupinga ufisadi na sera za watawala wa awali za kujisalimisha kwa seriali ya Paris kwa hakika lilikuwa tangaza la mwisho wa ukoloni mamboleo wa Ufaransa katika baadhi ya nchi za bara la Afrika na mwanzo wa zama mpya za maisha ya kisiasa na kiuchumi katika nchi tofauti za Kiafrika.
Siku kadhaa zilizopita, "Catherine Colonna", Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, alikiri rasmi kwamba wimbi la chuki dhidi ya Ufaransa limeanza tena barani Afrika. Ukweli ni kwamba, kutokana na ongezeko la mwamko wa kisiasa na kijamii, nchi za Kiafrika, hasa katika miongo ya hivi karibuni, sio tu kwamba hazikubali tena uingiliaji wowote wa kisiasa na kijeshi katika masuala ya ndani ya nchi hizo, lakini pia zinataka rasmi kukomeshwa sera za kijeshi za Ufaransa barani Afrika.

Katika mazingira hayo mapya, Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya sio tu kwamba haziwezi tena kuendelea kuwepo kijeshi na kupora maliasili na madini ya nchi za Kiafrika kama dhahabu na kadhalika, bali zinalazimika kukubali zama mpya za mahusiano yenye msingi wa kuheshimiana. Ukweli huo umeashiriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad pale aliposema: "Ufaransa lazima sasa itambua kuwa Chad imekua na kukomaa."